Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisha mapigano Ukraine kupisha uchunguzi:UN 

Wagonjwa kwenye wadi hospitalini Kyiv, Ukraine.
©WHO/Anastasia Vlasova
Wagonjwa kwenye wadi hospitalini Kyiv, Ukraine.

Sitisha mapigano Ukraine kupisha uchunguzi:UN 

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umetaka kusitishwa mapigano mara moja nchini Ukraine ili kupisha uchunguzi wa vifo vya raia vilivyotokea Bucha karibu na mji mkuu Kyiv.

Taarifa ya mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Misaada ya Kibinadamu Osnat Lubrani kwa niaba ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine inasema wamesikitishwa na picha zilizo sambaa zinazo onesha watu wameuwawa pamoja na uwepo wa ripoti za unyanyasaji wa kutisha dhidi ya raia wanaume, wanawake na watoto huko Bucha, Irpin, na Hostomel karibu na Kyiv na katika maeneo mengine ya Ukraine.

Salamu za rambirambi kutoka kwa Katibu Mkuu wa UN

Taarifa hiyo imerudia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wa kusitisha mapigano mara moja na kuruhusu  uchunguzi huru utakaowezesha uwajibikaji.

“Nimeshtushwa sana na picha za raia waliouawa huko Bucha, Ukraine. Ni muhimu kwamba uchunguzi huru ulete uwajibikaji wenye ufanisi. “ amesema Katibu Mkuu Guterres 

Umoja wa Mataifa pia umetuma salamu za rambirambi kwa wafiwa. “Tunajua kwamba maneno pekee hayawezi kufariji kufiwa na wapendwa au kuchukua nafasi ya vitendo wanavyopitia. Vita hivi vya kuua vinahitaji kukomeshwa kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kumaliza upotevu huu usio na maana wa maisha na mateso kwa watu.

Ukiukwaji wa haki za binadamu

Ripoti na video zilizosambaa zinaibua maswali kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu ndio maana taarifa hiyo imesisitiza ni muhimu na kwa haraka kuwa na uchunguzi huru ili kubaini ukubwa wa uhalifu na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.

Taarifa imemnukuu Lubrani akieleza ni muhimu ripoti zote za unyanyasaji dhidi ya raia zidhibitishwe kwa uhuru.

Ameongeza kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia masuala ya haki za kibinadamu nchini Ukraine unajaribu kutembelea maeneo hayo bila kuchelewa na kuahidi kuwa “Mtu yeyote ambaye amejihusisha na unyanyasaji dhidi ya raia lazima awajibishwe chini ya haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu.”

Matumizi ya silaha za vilipulizi huleta madhara kwenye makazi ya raia kama pichani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv ambapo msichana anaonekana akistaajabu shambulizi mbele ya jengo la nyumba, shambulizi lililofanywa na operesheni za kijeshi zinazoendelea.
UNICEF/Anton Skyba for The Globe and Mail
Matumizi ya silaha za vilipulizi huleta madhara kwenye makazi ya raia kama pichani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv ambapo msichana anaonekana akistaajabu shambulizi mbele ya jengo la nyumba, shambulizi lililofanywa na operesheni za kijeshi zinazoendelea.

Bachelet asema makaburi yafukuliwe

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametoa taarifa akisema ameshtushwa na picha za raia wakiwa wamekufa barabarani na kwenye makaburi yaliyotengenezwa  katika mji wa Bucha nchini Ukraine naye ametaka uchunguzi huru na madhubuti wa kile kilichotokea ili kuhakikisha ukweli, haki, uwajibikaji, pamoja na fidia na tiba kwa familia walioathirika.

 "Ripoti zinazoibuka kutoka eneo hili na zingine zinazua maswali mazito na ya kutatanisha kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita, ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu," alisem Bachelet na kuongeza kuwa. "Ni muhimu kwamba miili yote ifukuliwe na kutambuliwa ili familia za watu waliozikwa zifahamishwe, na sababu haswa za kifo zibainishwe. Hatua zote zinapaswa kuchukuliwa ili kuhifadhi ushahidi."

Daktari akitembelea kwenye eneo lililo handakini ambako anaficha wagonjwa dhidi ya mashambulizi. Hapa ni katika hospitali ya Wilaya ya Kati huko Brovary, Ukraine
© WHO/Anastasia Vlasova
Daktari akitembelea kwenye eneo lililo handakini ambako anaficha wagonjwa dhidi ya mashambulizi. Hapa ni katika hospitali ya Wilaya ya Kati huko Brovary, Ukraine

Sheria na wajibu wakati wa vita

Mratibu mkazi huyo wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wana makubaliano na wajibu kwa raia chini ya mkataba wa Geneva iwe kipindi cha amani au wakati wa vita

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine itaendelea kufuatilia kwa karibu na kuripoti juu ya mashambulizi dhidi ya shule, hospitali, wafanyakazi wa afya pamoja na miundombinu mingine ya kiraia, ili kuona matumizi ya silaha nzito katika maeneo ya makazi ya raia na kunyimwa kwa misaada ya kibinadamu.

Wananchi wa Ukraine wamekuwa  wakiishi katika vita kwa mwezi mmoja sasa huku watoto , wanawake, walemavu na wazee wakizidi kuteseka kwakukosa mahitaji muhimu . Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa mapigano ili waweze kufikishiwa misaada ya kibinadamu na raia waweze kuondoka kwa usalama.