Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bahari ni uhai, sio kwangu mimi tu bali kwa Wakenya wote: Bernadatte Loloju 

Samaki wakiogelea katika Bahari ya Sham
© Ocean Image Bank/Brook Peters
Samaki wakiogelea katika Bahari ya Sham

Bahari ni uhai, sio kwangu mimi tu bali kwa Wakenya wote: Bernadatte Loloju 

Tabianchi na mazingira

Katika kuelekea siku ya bahari duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Juni 8 tutakuletea sauti za watu mbalimbali wakizungumzia kwa nini bahari ni muhimu kwao. Maudhui ya mwaka huu ya siku ya bahari ni “kuhuisha hatua ya pamoja kwa ajili ya bahari” ikichagiza serikali, mashirika, asasi za kiraia na wadau wote kuchukua hatua ili kuilinda bahari na rasilimali zake kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo .

Na katika kusisitiza umuhimu huo wa bahari leo tunaanzia Kenya kaunti ya Samburu kwa mwananchi Bernadatte Loloju akieleza kwa nini bahari ni muhimu kwake na kwa Wakenya wote “Bahari kwangu inamaanisha uhai , kwasababu ya nini ninasema uhai, kwa sababu uhai wa samaki na vitu vyote Mungu alivyoumba ambavyo viko chini ya maji vinahitaji kulindwa na kuhakikishwa viko chini ya bahari, kwa hivyo vinaletea uhai wanyama na binadamu. Na sisi tukiwa wakenya na mimi nikiwa mkaazi wa Samburu na mkaazi wa Nairobi naweza kupata vitu vingi kupitia baharini, kwa sababu meli zinakuja na zinatuletea vitu vingi sana.”  

Mbali ya biashara kubwa ambayo inawasaidia Wakenya wengi kupitia bahaii Bernadatte anasema bahari pia ni kivutio cha sekta ya utalii wa nje na hata ndani ya nchi ambao naye ni mteja mkubwa “Kwa hivyo mimi nafurahia bahari kabisa na wakati naenda Mombasa ninaogelea ninafurahia kuonna viumbe wa baharini na hivyo ndio maana nasema tuweze kuhakikisha bahari zetu zinashughulikiwa na hazijaharibiwa kwa sababu ni uhai.”