Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa hewa chafuzi: Mataifa lazima yaende mbali zaidi kuliko ahadi za sasa - UNEP

Vijana wanaharakati wa tabianchi huko Maldives wakipaza sauti zao wakihimiza hatua za kukuza mazingira zichukuliwe..
© UNICEF/Pun
Vijana wanaharakati wa tabianchi huko Maldives wakipaza sauti zao wakihimiza hatua za kukuza mazingira zichukuliwe..

Uzalishaji wa hewa chafuzi: Mataifa lazima yaende mbali zaidi kuliko ahadi za sasa - UNEP

Tabianchi na mazingira

Wakati joto la ulimwengu na uzalishaji wa hewa chafuzi vikivunja rekodi katika mwaka huu wa 2023, Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) ya Pengo la Uzalishaji hewa chafuzi iliyotolewa leo Novemba 20 mjini Nairobi Kenya imeeleza kwamba imegundua kuwa ahadi za sasa chini ya Mkataba wa Paris zinaweka ulimwengu kwenye mstari wa ongezeko la joto la nyuzi joto 2.5 hadi 2.9 za Selsiasi zaidi ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda katika karne hii.

Ripoti hii iliyotolewa kuelekea mkutano wa tabianchi wa mwaka 2023 unaotarajiwa kufanyika huko Dubai, Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwezi huu, inaashiria hitaji la dharura la kuongezeka kwa hatua za kukabiliana na tabianchi kwani rekodi ya viwango vya juu vya joto ilivunjwa na kufikia kiwango kipya mwaka huu lakini wakati huo huo kwa mara nyingine tena ulimwengu umeshindwa kupunguza uzalishaji wa chafuzi.  

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Anderson akisisitiza kuchukua hatua mpya za kudhibiti mwenendo mbaya wa ulimwengu anasema, "Hakuna mtu au uchumi uliosalia kwenye sayari bila kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tunahitaji kuacha kuweka rekodi zisizohitajika kuhusu uzalishaji wa hewa chafuzi, joto la juu duniani na hali mbaya ya hewa.” 

mitambo ya nishati kisukuku kama vile petroli na dizeli ndio inayoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi
© Unsplash/Marcin Jozwiak
mitambo ya nishati kisukuku kama vile petroli na dizeli ndio inayoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi

Viongozi katika COP28 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake alioutoa akiwa New York, Marekani amesema yote haya ni kushindwa kwa uongozi duniani, usaliti kwa wanyonge, na fursa kubwa iliyopotea. 

Guterres anasisitiza uelekeo wa nishati ya jadidifu akisema, “Tunajua bado inawezekana kufanya kikomo cha nyuzi joto 1.5 za Selsiasi kuwa ukweli. Na tunajua jinsi ya kufika huko - tuna ramani kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati na Jopo la serikali (duniani) kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC. Inahitajika kung'oa mzizi wenye sumu wa janga la tabianchi: nishati ya mafuta ya kisukuku.” 

Kiongozi huyu wa Umoja wa Mataifa anawataka viongozi kuimarisha juhudi zao kwa kiasi kikubwa sasa, wakiwa na matamanio ya juu, hatua za juu na kuweka rekodi za juu za upunguzaji wa hewa ukaa. “Awamu inayofuata ya mipango ya kitaifa ya tabianchi itakuwa muhimu.” Anasema Guterres na kuongeza kuwa, “Mipango hii lazima iungwe mkono na fedha, teknolojia, usaidizi na ushirikiano ili kuifanya iwezekane. Kazi ya viongozi katika COP28 ni kuhakikisha hilo linafanyika.” 

Halijoto imefikia rekodi ya juu kote ulimwenguni mnamo 2023.
© Unsplash/John Towner
Halijoto imefikia rekodi ya juu kote ulimwenguni mnamo 2023.

Rekodi zilizovunjwa mwaka 2023 

Hadi mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, siku 86 zilirekodiwa kuwa na joto ya zaidi ya nyuzi joto 1.5 za Selsiasi juu ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda. Septemba ulikuwa mwezi wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa, ukiwa na wastani wa halijoto duniani nyuzi 1.8 za selsiasi juu ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda. 

Ripoti hiyo imegundua kuwa uzalishaji wa hewa chafuzi duniani (GHG) umeongezeka kwa asilimia 1.2 kutoka 2021 hadi 2022 hadi kufikia rekodi mpya ya Gigatonnes 57.4 ya ‘Carbon Dioxide Equivalent’ (GtCO2e). Uzalishaji wa GHG kote katika nchi za G20 uliongezeka kwa asilimia 1.2 mwaka wa 2022. Mitindo ya utoaji wa hewa chafuzi inaonesha mifumo ya kimataifa ya ukosefu wa usawa. Kwa sababu ya mienendo hii inayotia wasiwasi na juhudi zisizotosheleza za kupunguza hali hiyo, dunia iko kwenye mwelekeo wa kupanda kwa joto zaidi ya malengo ya tabianchi yaliyokubaliwa katika karne hii. 

Ripoti hii inatoa wito kwa mataifa yote kuwasilisha mabadiliko ya maendeleo ya viwango vya chini vya hewa ukaa kwa kuzingatia mabadiliko ya nishati. Makaa ya mawe, mafuta na gesi inayochimbwa katika kipindi chote cha uzalishaji kwenye migodi vinaweza kuzalisha zaidi ya mara 3.5 ya bajeti ya hewa ukaa inayopatikana ili kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5 za Selsiasi, na karibu bajeti yote iliyopo kwa nyzi joto 2 za Selsiasi. 

Nchi zilizo na uwezo na wajibu mkubwa wa uzalishaji wa hewa chafuzi - hasa nchi zenye mapato ya juu na zinazotoa hewa chafuzi nyingi miongoni mwa G20 - zitahitajika kuchukua hatua kabambe zaidi na za haraka na kutoa usaidizi wa kifedha na kiufundi kwa mataifa yanayoendelea. Kwa vile nchi za kipato cha chini na cha kati tayari zinachangia zaidi ya theluthi mbili ya uzalishaji wa GHG duniani, kukidhi mahitaji ya maendeleo na ukuaji wa uzalishaji mdogo wa hewa chafuzi ni kipaumbele katika mataifa kama hayo - kama vile kushughulikia mifumo ya mahitaji ya nishati na kuweka kipaumbele kwa minyororo ya usambazaji wa nishati safi.