Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC imeiondoa kesi dhidi ya Vincent Otti

Mwaka 2004 Kaskazini mwa Uganda wasafiri wa usiku walikuwa wanaondoka majumbani mwao na kukaa makazi ya muda kwa hofu kwamba watoto hao wataingizwa kwenye LRA.
© UNICEF/Chulho Hyun
Mwaka 2004 Kaskazini mwa Uganda wasafiri wa usiku walikuwa wanaondoka majumbani mwao na kukaa makazi ya muda kwa hofu kwamba watoto hao wataingizwa kwenye LRA.

ICC imeiondoa kesi dhidi ya Vincent Otti

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) hii leo imetangaza kuiondoa kesi dhidi ya anayedaiwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Mnadhimu wa Pili kikundi cha waasi cha Lord’s Resistance Army, LRA nchini Uganda, Vincent Otti kufuatia ‘Ombi la Tatu la Mwendesha Mashtaka Kufuta Kesi dhidi ya Vincent Otti’.

 

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mwendesha Mashtaka kueleza kuwa “ushahidi wote uliopo unaonesha Bw Otti aliuawa mwezi Oktoba 2007 huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC”.

Mbali na maelezo yaliyowasilishwa hapo awali mbele ya Mahakama, Mwendesha Mashtaka aliambatanisha taarifa mbili za mashahidi na kueleza kuwa shahidi wa pekee wa mauaji ya Bw Otti lazima achukuliwe kuwa amekufa na kwamba hatua zaidi za uchunguzi haziwezi kusababisha uthibitisho wowote wa kifo cha Bwana Otti.

Katika uamuzi wake, Mahakama ya ICC iligundua uamuzi pekee wa kuridhisha ni kwamba Bw Otti hayuko hai tena na kwamba Mahakama haiwezi kuwa na mamlaka juu ya mtu aliyefariki dunia kwa hivyo kifo cha mshukiwa kilihitajika kumaliza kesi dhidi ya Bw Otti, ambapo hati zote muhimu, pamoja na hati zozote za kukamatwa, hutolewa bila athari.

Kuhusu kesi dhidi ya Vincent Otti

Hati ya Kukamatwa kwa Vincent Otti ilitolewa tarehe 8 Julai 2005 na kufunguliwa tarehe 13 Oktoba 2005. 

Bwana Otti alikuwa akishukiwa kwa makosa 11 ya uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo (mauaji, utumwa wa kingono, vitendo vya kinyama vya kuumiza vibaya watu kimwili na kuwatesa) na makosa 21 ya uhalifu wa kivita yakijumuisha (ubakaji, kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia  kwa makusudi, kuandikishwa watoto kwa lazima katika vita, kuwatendea ukatili raia, wizi na mauaji). Mashambulizi haya yanadaiwa kufanywa kaskazini mwa Uganda baada ya 1 Julai mwaka 2002. 

Kesi ya Bw Otti iliunganishwa kwenye kesi ya makamanda wengine wa LRA ambao ni Joseph Kony na Dominic Ongwen

Tarehe 6 Februari 2015, Chumba cha Utangulizi cha II kilifuta kesi dhidi ya Dominic Ongwen kutoka kwa Kony na wenzake kufuatia kujisalimisha kwake chini ya ulinzi wa ICC tarehe 16 Januari 2015.