Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

E4J ndio mwelekeo wa kunusuru vijana - Mutombo

Dikembe Mutombo, Rais wa Mfumo wa Dikembe Mutombo na pia mcheza kikapu mashuhuru wa NBA ambaye sasa amestaafu. Pichani akiwa katika vikao maalum kwenye makao makuu ya UN kuhusu uzuiaji uhalifu, Aprili 2018
UN /Manuel Elias
Dikembe Mutombo, Rais wa Mfumo wa Dikembe Mutombo na pia mcheza kikapu mashuhuru wa NBA ambaye sasa amestaafu. Pichani akiwa katika vikao maalum kwenye makao makuu ya UN kuhusu uzuiaji uhalifu, Aprili 2018

E4J ndio mwelekeo wa kunusuru vijana - Mutombo

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Balozi wa kimataifa wa chama cha mpira wa kikapu nchini Marekani,  NBA, Dikembe Mutombo amesema kuwapatia vijana elimu inayowawezesha kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani ni suala mujarabu katika kutekeleza lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs linalohusu amani, haki na taasisi thabiti.

Bwana Mutombo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema hayo alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kushiriki mkutano ulioandaliwa na Qatar na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC ukiangazia mpango wa elimu kuhusu haki, E4J.

Mcheza mpira huyo wa kikapu mashuhuri ambaye sasa amestaafu akasema kufanikisha Elimu kuhusu haki kuna mengi ya kufanya akisema, “Elimu bado ni ufunguo wa mafanikio, lakibni michezo nayo ina dhima yake. Iwapo utawarushia mpira wa kucheza vijana wetu wanapotoka darasani saa saba, unaweza kuweka mawazo yao na jambo la kufanya kabla ya kufanya kazi za shule. Wanaweza kufirikia kushinda mchezo, mazoezi na kuwa na marafiki zao  badala ya kubeba bunduki na silaha na kwenda kufanya mambo mabaya.”

 Alipoulizwa ujumbe wake kwa vijana, Mutombo ambaye anaongoza taasisi ya Mutombo huko nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema, “mustakhbali wa dunia yetu uko mikononi mwao. Sisi ambao tumekuja kabla yao tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu ili kuandaa dunia hii tuyyolipewa ili iwe pahala bora kwa kizazi kijacho. Ni lazima wafuate utawala wa sheria na kuheshimu sheria ambazo zimekuwa zinatumika kwenye bara hili na ulimwenguni.”

Mpango wa E4J, ni  mojawapo ya mipango minne ya programu ya utekelezaji wa azimio la Doha lililopitishwa mwezi Aprili mwaka 2015 mwishoni mwa mkutano wa 13 wa Baraza la kimataifa la kuzuia uhalifu na kuzingatia sheria.

Watoto wakicheza  nje ya moja ya shule za muda huko eneo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto wakicheza nje ya moja ya shule za muda huko eneo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

UNODC na wadau wake ikiwemo Qatar ambayo inafadhili mpango huo, wanaamini kuwa kwa kuunganisha nguvu na uelewa wa wataalamu mbalimbali na kuhakikisha kuna vifaa vinavyotakiwa, “kuelimisha kuhusu utii wa sheria na udhibiti wa uhalifu katika ngazi zote za elimu kuanzia shule ya msingi hadi chuo Kikuu ni hatua muhimu ya kuwa na raia wema wanaowajibika kwa jamii zao.”

Mipango mingine ni maadili kwenye mahakama, uraghibishaji wa wafungwa na kutumia michezo kuepusha uhalifu.

E4J unaamini kuwa elimu kwa vijana wa sasa itatoa hakikisho la kesho iliyo bora zaidi.

Mapema akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Yuri Fedotov amerejelea kile ambacho nchi wanachama waliridhia katika mkutano wa 13 uliopitisha azimio la Doha, akisema kuwa, “ nchi wanachama ziliridhia kuwa elimu kwa watoto wote na vijana ni msingi wa kuzuia uhalifu na rushwa na kuendeleza utamaduni wa utii wa sheria unaounga mkono utawala wa sheria na haki za binadamu.”

Katika ngazi ya shule ya msingi, E4J inalenga kuelimisha watoto maadili ya heshima utu, usawa na kujikubali ambapo wanatumia mbinu mbalimbali ikiwemo mfululizo wa mchezo wa vikaragosi uitwao  ‘the Zorbs.” Katika mchezo huu vikaragosi hao wametumia stati na maadili yao kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo.