Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatiwa hofu kubwa na mauaji ya raia wa kabila la Masalit Sudan - OHCHR

Mtoto amesimama na maji yaliyokusanywa kutoka kambi ya IDP huko Nyala, Darfur. (Maktaba)
© UNICEF/Zehbrauskas
Mtoto amesimama na maji yaliyokusanywa kutoka kambi ya IDP huko Nyala, Darfur. (Maktaba)

Tunatiwa hofu kubwa na mauaji ya raia wa kabila la Masalit Sudan - OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR leo imesema inatiwa wasiwasi mkubwa na kusikitishwa sana na ripoti kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF nchini Sudan na wanamgambo washirika wao wa Kiarabu waliua mamia ya raia wa kabila la Masalit katika mji wa Ardamata mapema mwezi huu, katika shambulio lingine lililochochewa na misingi ya kikabila dhidi ya raia wasio Waarabu wa Masalit huko Darfur Magharibi katika miezi michache tu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis msemaji wa OHCHR Jeremy Laurence amesema “Taarifa za awali ambazo tumezipata kutoka kwa walionusurika na mashahidi zinaonyesha kwamba raia wa Masalit waliteseka kwa siku sita za ugaidi mikononi mwa RSF na wanamgambo washirika wake baada ya kuchukua udhibiti wa kambi ya jeshi la Sudan huko Ardamata tarehe 4 Novemba.”

Kituo hicho kiko nje kidogo ya El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi na ofisi hiyo inasema “Baadhi ya waathiriwa waliuawa kwa pamoja au kuchomwa moto wakiwa hai. Wengi wa waliouawa walikuwa vijana wa Kimasalit na jamaa za wanajeshi wa Sudan waliosalia Ardamata, baada ya wanajeshi hao kuukimbia mji huo.”

Pia imesema wanawake na wasichana waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia katika kambi ya wakambizi wa ndani ya Ardamata na katika baadhi ya nyumba.

Wakimbizi kutoka Darfur wakiwa wamekusanyika kwenye kambini baada ya kuvuka mpaka kutoka Sudan na kuingia Chad
© UNHCR/Jutta Seidel
Wakimbizi kutoka Darfur wakiwa wamekusanyika kwenye kambini baada ya kuvuka mpaka kutoka Sudan na kuingia Chad

Maelfu wametawanywa 

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa ofisi ya haki za binadamu “Maelfu ya watu wameyahama makazi yao, wengine wakivuka mpaka na kuelekea Chad.”

Ameongeza kuwa “Wakiangazia kambi mbili za wakimbizi wa ndani za Ardamata na Dorti kitongoji cha Al-Kabri, ambacho kinakaliwa na Wamasalit, RSF na wanamgambo washirika wao waliripotiwa kupora mali, kuwatesa wakimbizi wa ndani, na kuwaua wengi wao kabla ya kuacha miili yao bila kuzikwa ikizagaa mitaani.”

Ameongeza kuwa tarehe 5 Novemba pekee, wanaume 66 wa Masalit waliuawa kwa katika matukio matatu tofauti. 

“Katika wilaya ya Al-Kabri, wanaume walitenganishwa na wanawake na kuuawa. Mamia zaidi ya wanaume walikamatwa na kupelekwa katika kambi mbalimbali za kizuizini zinazoendeshwa na RSF. Hatima yao na waliko bado haijulikani.” Amesema.

Shambulio la Ardamata imesema ofisi ya haki za binadamu kuwa ni shambulio la pili lililoripotiwa na RSF na wanamgambo wake wa Kiarabu dhidi ya raia wa Masalit katika kipindi cha miezi kadhaa. 

“Kati ya Mei na Juni 2023, mamia ya wanaume, wanawake, na watoto wa Masalit ikiwa ni pamoja na gavana wa Darfur Magharibi waliuawa. Wengi wao walizikwa katika makaburi ya pamoja huku miili ya wengine ikiachwa mitaani. Mashambulizi kama haya yanaweza kuwa uhalifu chini ya sheria za kimataifa.”

Watu wanaendelea kuhama makazi yao kutokana na vita nchini Sudan.
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Watu wanaendelea kuhama makazi yao kutokana na vita nchini Sudan.

Shutma za madai ya kulipiza kisasi

Pia ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema “Kuna madai mazito kwamba katika mashambulizi ya kulipiza kisasi, baadhi ya raia wa Kiarabu waliripotiwa kushambuliwa na baadhi ya wanamgambo wa Masalit. Ukiukaji wote lazima ukomeshwe mara moja, na wale waliohusika lazima wafikishwe mahakamani kufuatia uchunguzi wa kina, huru na usio na upendeleo.”

Ofisi hiyo imesisitiza kwamba “Tunarejelea wito wa Kamishna Mkuu Volker Türk wa mwezi Juni kuhusu uongozi wa RSF kulaani na kukomesha mauaji, ghasia nyinginezo na kauli za chuki zinazolenga raia, kwa kuzingatia makabila yao.”

Huku kukiwa na ripoti za kutisha za kutokea kwa shambulio linalokaribia la RSF dhidi ya El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, “tunawakumbusha wao na wahusika wengine wote kwenye mzozo kuheshimu wajibu wao wa sheria za kimataifa za kibinadamu ili kuhakikisha ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia.” Imesema OHCHR.