Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yamfunga jela kamanda wa waasi nchini Uganda 

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ICC, imemuhukumu kifungo cha miaka 25 jela kiongozi wa zamani wa LRA, Dominic Ongwen.
© ICC-CPI
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ICC, imemuhukumu kifungo cha miaka 25 jela kiongozi wa zamani wa LRA, Dominic Ongwen.

ICC yamfunga jela kamanda wa waasi nchini Uganda 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC imemhukumu kifungo cha miaka 25 jela kamanda wa zamani wa kikundi cha waasi cha Lord’s Resistance Army, LRA nchini Uganda, Dominic Ongwen. Hukumu hiyo dhidi ya Ongwen mwenye  umri wa miaka 45, imetolewa leo huko The Hague Uholanzi kufuatia kamanda huyo wa zamani kupatikana na hatia ya makosa 61tarehe 4 mwezi Februari mwaka huu. 

Makosa hayo yanajumuisha uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa Kaskazini mwa Uganda kati ya tarehe 1 Julai 2002 na 31 Desemba 2005.  

Mathalani makosa ya uhalifu wa kingono na wa kijinsia aliowatendea wasichana na wanawake ndani ya brigedi ya Sinia, uhalifu ambao ni ndoa ya kulazimishwa, mateso, ubakaji, utumwa wa kijinsia na utumwa.  

Pia alitumikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 15 katika kikosi cha Sinia na kuwatumia kushiriki kikamilifu katika ukatili.  

Akisoma hukumu hii leo, Jaji Kiongozi wa jopo la majaji Bertram Schmitt amesema kipindi cha uwepo wake rumande tangu tarehe 4 mwezi Januari 2015 hadi tarehe 6 mwezi huu wa Mei mwaka 2021 kitapunguzwa kwenye hukumu hiyo. 

Halikadhalika mhukumiwa ana fursa ya kukata rufaa kupitia mahakama ya rufaa ya ICC. 

Akifafanua zaidi kwenye hukumu hiyo, Jaji Schmitt amesema katika uamuzi wao wamekumbwa na mazingira ya kipekee ya mshtakiwa ambaye kwa utashi wake alitenda mambo ya kikatili na machungu kwa waathirika. 

Na wakati huo huo walikuwa na mazingira ya mshtakiwa mwenyewe ambaye awali alikumbwa na machungu mbele ya watesi wa kundi hilo la LRA ambapo baadaye yeye aligeuka na kuwa mwanachama mashuhuri na kisha kiongozi. 

Jopo liliamua kukubali kupatia uzito wa hoja ya mazingira ya kwamba utoto wa Ongwen ulikuwa wa machungu chini ya mikono ya LRA na maisha yake ndani ya kikundi hicho cha waasi akiwa mtoto. 

Hata hivyo jopo la majaji lilikataa utetezi wa upande wa mshtakiwa, likirejelea uamuzi wake wa tarehe 4 mwezi Februari mwaka huu wa 2021, na kuzingatia kuwa mazingira ya kupunguza hukumu kwa madai kuwa uwezo wake wa kufikiria ulipunguzwa kwa kuteswa akiwa mtoto, hayawezi kutumika kwa sasa. 

Jopo hilo pia limekataa hoja ya kwamba kutaka kupatiwa kipaumbele mfumo wa kijadi wa haki, likisema kuwa hakuna uwezekano wa kubadili hukumu ya ICC itekelezwe kijadi.