Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Mashariki: Zaidi ya watu milioni 50 kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka
FAO/IFAD/WFP/Michael Tewelde
Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka

Afrika Mashariki: Zaidi ya watu milioni 50 kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Tabianchi na mazingira

Zaidi ya watu milioni 50 wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula (IPC Awamu ya 3 au zaidi*) mwaka huu 2022 katika nchi saba za IGAD (Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda) kwa mujibu wa toleo la mwaka 2022 la Mtazamo wa Kikanda wa IGAD kuhusu Majanga ya Chakula iliyotolewa leo. 

“Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, na Sudan zinakabiliwa na janga kubwa zaidi la chakula katika eneo hilo.” Imesema taarifa ya pamoja ya FAO, WFP na IGAD iliyotolewa hii leo mjini Addis Ababa, Ethiopia.  

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa takriban watu 300,000 wanatarajiwa kukabiliwa na Janga la njaa la juu ngazi ya 5 (IPC Awamu ya 5*) nchini Somalia na Sudan Kusini mwaka huu 2022, huku Hatari ya Njaa ikitokea katika maeneo manane ya Somalia hadi Septemba katika tukio la kushindwa kwa uzalishaji wa mazao na mifugo, kuongezeka kwa gharama za chakula na kwa kukosekana kwa misaada ya kibinadamu iliyopunguzwa. 

Hali ya mwaka huu 2022, watu milioni 50 hadi 51 wakitarajiwa kukabiliwa na Janga au njaa mbaya zaidi (IPC Awamu ya 3 au zaidi*), inaashiria ongezeko kubwa kutoka mwaka 2021 wakati watu milioni 42 walikumbwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula. Mwaka jana 2021, eneo la IGAD lilichangia karibu asilimia 22 ya idadi ya watu duniani katika Janga au njaa mbaya zaidi (IPC Awamu ya 3 au zaidi*), huku takriban watoto milioni 10 walio chini ya umri wa miaka 5 wakikabiliwa na utapiamlo mkali. Aidha, asilimia 24 ya wakimbizi wa ndani milioni 51 duniani walikuwa pia katika nchi za IGAD, hasa Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Sudan. 

"Eneo letu limeathiriwa zaidi kuliko hapo awali", anasema Workneh Gebeyehu, Katibu Mtendaji IGAD akiongeza kuwa "mchanganyiko wa hali mbaya ya tabianchi, migogoro, na changamoto za uchumi mkuu hufanya iwe vigumu kwa jumuiya zetu kuhimili mitikisiko mingi. Takwimu tunazotoa leo ni za kuhuzunisha, na nina wasiwasi kwamba zinaweza kuongezeka zaidi kwani matarajio ya msimu wa mvua wa Oktoba hadi Desemba ni mbaya."