Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Miji Duniani: Viongozi watoa ujumbe kuhamasisha ufadhili

Miji endelevu inasaidia katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Unsplash/chuttersnap
Miji endelevu inasaidia katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Siku ya Miji Duniani: Viongozi watoa ujumbe kuhamasisha ufadhili

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni Siku ya Miji Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN Habitat), kila mtu kwa namna yake amesisitiza ushirikiano katika kufadhili miji endelevu.

Bwana Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa siku hii ametoa wito kwamba, ‘tunapoadhimisha Siku ya Miji Duniani, “tuazimie kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maeneo ya mijini ambayo si tu ni injini za ukuaji, bali vinara wa uendelevu, mnepo, na ustawi kwa wote.”

“Siku ya Miji Duniani ni wakati wa kuzingatia jukumu muhimu la miji katika maendeleo endelevu.” Ndivyo alivyouanza ujumbe wake kiomgozi huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Guterres anayasema haya akiwa na angalizo kwamba, mamlaka za mitaa zinapambana na usaidizi mdogo na rasilimali, wakati mahitaji ya miundombinu, nyumba za bei nafuu, usafiri bora, na huduma za kijamii ni kubwa na inakua. “Kaulimbiu ya mwaka huu, Kufadhili Maendeleo Endelevu ya Miji, ni wito wa kuchukua hatua,” Anafafanua.

Serikali, mashirika ya kimataifa, sekta ya kibinafsi, na jumuiya za kiraia, lazima zifanye kazi pamoja ili kuhamasisha fedha kwa ajili ya miji imara na endelevu. “Mimi ni mtetezi mkubwa wa suluhisho za ufadhili katika ngazi ya kimataifa. Hizi lazima zitumike, pamoja na vyanzo bunifu na tofauti vya ufadhili, ili kuimarisha mikakati ya ufadhili wa ndani ambayo ni rafiki wa tabianchi, jumuishi na sawa.” Anasema Guterres.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN Habitat), Maimunah Mohd Sharif akisisitiza Kaulimbiu ya mwaka huu, Kufadhili Mstakabali wa Miji Endelevu kwa wote, amesema unahitajika mfumo mpya wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo endelevu ya miji na kwamba pia inahitajika kuwekeza katika upangaji jumuishi na kuongeza kasi ya kuyafanya makazi na nyumba kuwa haki ya binadamu.