Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji ndio kitovu cha kufanikisha SDGs- Katibu Mkuu UN

Ukuaji endelevu wa miji ni jawabu la kukabili mabadiliko ya tabianchi na huleta manufaa kwenye sekta za kiuchumi na kijamii ikiwemo elimu, usawa na mazingira
UN / Abdelmonem Makki
Ukuaji endelevu wa miji ni jawabu la kukabili mabadiliko ya tabianchi na huleta manufaa kwenye sekta za kiuchumi na kijamii ikiwemo elimu, usawa na mazingira

Miji ndio kitovu cha kufanikisha SDGs- Katibu Mkuu UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya miji duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka wakazi wa sayari dunia watambue dhima muhimu ya maeneo ya mijini katika kufanikisha malengo ya  maendeleo endelevu, SDGs. Thelma Mwadzaya na taarifa kamili.

Katika ujumbe wake wa siku hii inayoadhimishwa tarehe 31 mwezi Oktoba kila mwaka, Katibu Mkuu Guterres amesema mwaka ujao wa 2023 inasalia ngwe ya mwisho au nusu ya kufikia ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Anasema ingawa ng’we ya kwanza itakuwa imemalizika, bado taswira inagubikwa na kiza kinene kwenye malengo yote 17, hususan yale muhimu zaidi; kutokomeza umaskini na njaa, usawa wa jinsia na elimu, hakuna maendeleo badala yake ni kurudi nyuma.

Guterres anasema madhara ya kurudi nyuma badala ya kusonga mbele ni makubwa: Kuendelea kushamiri kwa janga la tabianchi, kuongezeka kwa umaskini, ukosefu wa usawa na mengine mengi.

Anasema, “lazima tubadili mwelekeo na tunaweza,” akitaja maudhui ya siku ya leo kuwa ni Chukua hatua za kieneo ili kwenda kimataifa kuwa yanadhihirisha ni kwa vipi malengo ya SDGs yana mtazamo wa kimataifa lakini utekelezaji wake unapaswa kuzingatia kwenye maeneo na kwamba utekelezaji kwa kiasi kikubwa unafanyika mijini.

Majawabu ya ajenda 2030 yanaanzia mijini

Amesema leo hii zaidi ya nusu ya wakazi wa dunia wanaishi mijini, na ifikapo mwaka 2050 zaidi ya theluthi mbili watakuwa wanaishi kwenye maeneo ya mijini.

Miji inazalisha zaidi ya asilimia 80 ya pato la dunia, halikadhalika asilimia 70 ya hewa chafuzi ya ukaa.

Guterres amesema miji mingi tayari inaongoza harakati za mpito kuelekea nishati isiyochafua mazingira na kuweka malengo na miundombinu inayohimili tabianchi.

Katibu Mkuu amesema “nasihi miji hiyo iendelee kushirikiana na serikali na miji rafiki duniani ili kubadilishana uzoefu na kusaidiana kuongeza malengo ya kuhimili tabianchi.”

Amesema hatua ambazo miji inachukua kuweka dunia endelevu kwa wote itakuwa na athari chanya dunia nzima na kwamba, “sera za marekebisho ambazo miji inaanzisha leo hii zinaweza kuchochea marekebisho yatakayookoa maisha na mbinu za kujipatia kipato kokote kule siku zijazo.”