Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waomboleza, bendera zapepea nusu mlingoti

Kufuatia ajali ya ndege Ethiopia Umoja wa Mataifa na mashirika yake yatapeperusha bendera, nusu mlingoti kwa ajili ya mshikamano na waliopoteza maisha kwenye ajali ya ndege.
UN Photo/Yih Peng Chia
Kufuatia ajali ya ndege Ethiopia Umoja wa Mataifa na mashirika yake yatapeperusha bendera, nusu mlingoti kwa ajili ya mshikamano na waliopoteza maisha kwenye ajali ya ndege.

Umoja wa Mataifa waomboleza, bendera zapepea nusu mlingoti

Masuala ya UM

Kufuatia ajali ya ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka mapema jana dakika sita tu baada ya kupaa kutoka uwanja wa kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa na kuwaua abiria wote, wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, salamu za rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka ofisi mbali mbali za Umoja huo.

Kuanzia Geneva Uswisi, Nairobi Kenya, Addis Abbaba Ethiopia, New York Marekani, Dar es Salaam Tanzania, Afghanistan na kwingineko kote ambako zipo ofis iza Umoja wa Mataifa na mashirika yake, siku ya leo imeanza kwa salamu nyingi za rambirambi kutokana na tukio hilo. 

Kutokana na maelekezo ya ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ofisi zote za Umoja wa Mataifa n azote zinazohusiana nazo kote duniani hii lieo zitapeperushwa nusu mlingoti ili kuwaenzi waliopoteza maisha.

NI MAJONZI MAKUBWA- GUTERRES

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani,  bendera ya umoja huo inapepea nusu mlingoti kuomboleza vifo vya wafanyakazi wake.

Majonzi ni dhahiri ambapo ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja huo, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 63 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema..

“Mlipokuwa mnaingia kwenye Umoja wa Mataifa hii leo mmeona bendera zote zinapepea nusu mlingoti. Hii bila shaka ni siku ya majonzi kwa wengi duniani, na hususan kwa Umoja wa Mataifa.”

 Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa huku akisema wanashirikiana na serikali kuhamasisha msaada na chochote kitakachohitajika na kwamba..

“Wafanyakazi wenzetu wanawake na wanaume kutoka kona mbalimbali duniani wakiwa na stadi mbalimbali, wote walikuwa na nia moja ya kuhudumia watu wote duniani na kufanya dunia pahala bora kwetu sote. Ni nia hiyo hiyo ambayo inatuleta kila siku kwenye Umoja wa Mataifa na imewaleta leo kwenye ukumbi huu leo. Tunapofungua mkutano huu muhimu , hebu tuenzi kumbukumbu za wafanyakazi wenzetu kwa kusongesha azma yao.”

Baada ya hotuba hiyo, wajumbe walisimama kwa dakika moja kukumbuka waliofariki dunia kwenye ajali hiyo.

TUMEPATA PIGO KUBWA- UNON

Mapema leo hii Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi Kenya, UNON, Bi Maimunah Mohd Sharif katika salamu zake za rambirambi amesema Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wamepata pigo kubwa.

Kupitia taarifa yake hiyo iliyotolewa mjini Nairobi Bi Maimunah amesema, “tunafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka kukusanya taarifa zaidi. Tunaungana na jumuiya ya kimataifa katika kuomboleza kupoteza maisha ya watu wengi, pamoja nan chi ambazo pia zimewapoteza raia wake katika ajali hii ya kusikitisha”

Leo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika ofisi mbalimbali ikiwemo ya Nairobi asubuhi kabla ya kuanza kazi za kila siku wametekeleza tukio la kukaa kimya kwa dakika moja ili kuwakumbuka wafanyakazi wenzao na marafiki waliopoteza maisha katika ndege hiyo Boeing 737 Max-8 ET302.

Aidha ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Nairobi imetangaza mawasiliano ya barua pepe unon-nairobiunic@un.org na nambari za simu +254 20 7623798 kwa ajili ya ndugu na marafiki wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao ianasadikika walikuwa katika ndege hiyo.

PUNDE TU BAADA YA AJALI JUMAPILI

Jana mara tu baada ya kuthibitika kutokea kwa ajali hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alituma salamu zake za rambirambi kwa srikali ya Ethiopia na watu wa Ethiopia akielezea kusikitishwa na ajali hiyo.

Aidha bwana Guterres kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika, “nimesikitidshwa sana na taarifa za asubuhi hii kuhusu kuanguka kwa ndege ya Ethiopia iliyowaua abiria wote. Rambirambi zangu ziwafikie familia na wamependwa wa waathirika wote wakiwemo wenzetu wa Umoja wa Mataifa ambao wamepotea katika ajali hii.”

MIONGONI MWA WALIOKUFA NI WAFANYAKAZI WA WFP

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakuka WFP, David Beasley aliutumia ukurasa wake twitter kuthibitisha kuwa WFP pia nayo  inaomboleza kwa kuwa maafisa wake walikuwa miongoni mwa abiria katika ndege hiyo, “tutafanya kila liwezekanalo kuzisaidia familia katika kipindi hiki kigumu. Tafadhali endeleeni kuwakumbuka na kuwaombea”

Wakuu wa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa Henrietta Fore ,Achim Steiner, Mark Lowcock na wengineo, wameendelea kutuma salamu za rambirambi kwa njia mbalimbali zikiwemo kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Ingawa shirika la ndege la Ethiopia bado halijatoa taarifa kamili kuhusu wat wote waliokuwemo katika ndege hiyo na pia kuhusu chanzo cha ajali, kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa jana na idara ya usalama ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya maafisa 21 wa Umoja wa mataifa wamefariki katika ajali hiyo. 

Taarifa hiyo imesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula (WFP) limepoteza maafisa sita, ofisi ya haki za binadamu (OHCHR) maafisa wawili na wawili kutoka ofisi ya muungano wa kimataifa wa mawasiliano (ITU). Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wahamiaji Sudan (IOM), Benki ya Dunia, na mpango wa Umoja wa mataifa nchini Somalia (UNSOM) kila moja limepoteza afisa mmoja. Pia maafisa sita wa Umoja wa Mataifa kutoka ofisi ya Nairobi (UNON) wamefariki.