Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi dhibitini mila potofu dhidi ya wanawake ikiwemo ubakaji wenye ualbino kwa madai ya kutibu VVU - CEDAW

Moja wa vikao vya wajumbe  wa kamati ya kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake CEDAW. (Maktaba)
UN
Moja wa vikao vya wajumbe wa kamati ya kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake CEDAW. (Maktaba)

Malawi dhibitini mila potofu dhidi ya wanawake ikiwemo ubakaji wenye ualbino kwa madai ya kutibu VVU - CEDAW

Wanawake

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) leo Jumatatu ya Oktoba, 30 imetoa matokeo ya uchunguzi wake baada ya kuzihoji nchi tisa ikiwemo Malawi. 

Matokeo yana pande mbili ambapo moja ni maeneo mazuri ambayo utekelezaji wa kila nchi wa Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake umefanyika, na pili ni maeneo ambayo yana mashaka na mapendekezo ya Kamati. 

Malawi 

Kwa nchi ya Malawi, Kamati imeeleza kuwa imesikitishwa na kuendelea kwa mila potofu dhidi ya wanawake na wasichana nchini humo, ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni na/au za kulazimishwa, mitala, “kusafisha wajane”, ukeketaji, pamoja na mila ya kuagiza ngono na wanawake na wasichana wenye ualbino kama tiba ya Virusi Vya Ukimwi, VVU. 

Kamati imetaka serikali kuimarisha juhudi zake za kupambana na mila potofu dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha kuwa wahalifu wanachukuliwa hatua na kuadhibiwa ipasavyo, na kwamba waathirika wanapata tiba madhubuti na ulinzi wa kutosha. 

Pamoja na hayo, Kamati imeipongeza Malawi kwa kumchagua Spika wa Bunge mwanamke wa kwanza mwaka 2019 na imezingatia ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Kitaifa na nyadhifa za mawaziri.  

Hata hivyo, Kamati imesalia na wasiwasi kuhusu kuendelea kwa mitazamo ya mfumo dume na mitazamo potofu ya kibaguzi inayozuia ushiriki wa wanawake katika maisha ya kisiasa na ya umma na uwakilishi mdogo wa wanawake katika nafasi za kufanya maamuzi katika utumishi wa umma. 

Kamati imependekeza kwamba Malawi ichukue hatua za kutoa ufadhili wa kampeni na kujenga uwezo juu ya ujuzi wa uongozi wa kisiasa kwa wagombea wanawake na kupitisha mgawo wa kijinsia kwa orodha za wapiga kura na miundo ya utendaji ya vyama vya siasa. 

Nchi nyingine zilizochunguzwa ni Albania, Bhutan, Ufaransa, Guatemala, Jamaica, Nicaragua, Ufilipino, na Uruguay. 

Kamati inasikitika kwamba Nicaragua haikujibu mawasiliano na haikutuma mjumbe kwenye majadiliano ya umma. Kamati iliamua kuendelea na uchunguzi dhidi ya Nikaragua bila kuwepo na wajumbe na ikatoa matokeo ya muda na mapendekezo ambayo yatafanywa kuwa ya mwisho katika kikao kijacho.