Skip to main content

Wanaotekeleza ukatili dhidi ya wanawke na walio na ulemavu wa ngozi wawajibishwe-OHCHR

Mlezi akimhudumia mtoto ambaye alitelekezwa huko Goma, Kivu Kaskazini nchini DRC. Mara nyingi watu wenye ulemavu wa ngozi wanakumbwa na vitisho na ukatili.
UN /Marie Frechon
Mlezi akimhudumia mtoto ambaye alitelekezwa huko Goma, Kivu Kaskazini nchini DRC. Mara nyingi watu wenye ulemavu wa ngozi wanakumbwa na vitisho na ukatili.

Wanaotekeleza ukatili dhidi ya wanawke na walio na ulemavu wa ngozi wawajibishwe-OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za bindamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imeelezea kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya ghasia za kisiasa, ukatili dhidi ya wanawake na mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Malawi, wakati huu uchaguzi ukitarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu wa 2019. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OHCHR, Rupert Colville ametaja baadhi ya matukio yaliyotekelezwa ikiwemo mbunge wa Malawi, Bon Kalindo ambaye alikamatwa kwa madai ya kumtukana rais ambapo baadaye aliachiwa huru lakini yaelezwa kuwa alivamiwa na wanaodaiwa kuwa vijana wanachama wa Democratic Progressive Party (DPP) kwenye makazi ya kamishna wa wilaya katika mji wa kusini wa Mulanje.

Ametolea mfano pia mashambulizi yaliyoelekezwa kwa wafuasi wa chama kimoja cha upinzani cha United Transformation Movement (UTM), uhalifu unaodaiwa kutekelezwa na vijana hao wa mrengo wa DPP.

Bwana Colville amesema ukatili umeongezeka tangu uchaguzi wa awali wa 2018, ambapo wagombea wanawake walikabiliwa na vitisho na mateso ikiwemo wapiga kura wanawake.

Aidha amekaribisha hatua ya rais Peter Arthur Mutharika ya mwezi huu ya kulaani ukatili wa kisiasa unaotekelezwa dhidi ya wanawake wanasiasa hatahivyo

“Tuna wasiwasi kwamba kufikia sasa hakuna mtu yeyote amewajibishwa kisheria kwa mashambulizi hayo yanayochochewa na siasa tangu yalipotekelezwa mwaka jana.”

Msemaji huyo amesema visa vya mashambulizi dhidi ya watu walio na ulemavu wa ngozi vimeongezeka kuelekea uchaguzi.

“Matukio ya hivi karibuni ni pamoja na mauaji ya Yasin Phiri, mwanamume wa miaka 55 aliyekuwa na ulemavu wa ngozi huko Kaskazini mwa Malawi Desemba 31 ambapo alidungwa kisu mbele ya mtoto wake kabla ya kutolewa nyumbani kwake na kukatwa mikono. Na siku tatu zilizopita Januari 22, mtoto wa mwaka mmoja alitekwa nyara na hajulikani aliko”.

Kwa mantiki hiyo OHCHR inatoa wito kwa mamlaka kuimarisha juhudi zake kulinsa watu walio na ulemavu wa ngozi na kuwashtaki na kuwawajibisha wanaodaiwa kutekeleza uhalifu huo.

 

TAGS:OHCHR, Malawi, uchaguzi, ukali dhidi ya wanawake, ulemavu wa ngozi