Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dkt. Tulia Ackson kutoka Tanzania ndiye Rais mpya wa IPU na mwanamke wa kwanza kutoka Afrika

Dkt. Tulia Ackson kutoka nchini Tanzania amechaguliwa kuwa Rais mpya wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani IPU.
IPU
Dkt. Tulia Ackson kutoka nchini Tanzania amechaguliwa kuwa Rais mpya wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani IPU.

Dkt. Tulia Ackson kutoka Tanzania ndiye Rais mpya wa IPU na mwanamke wa kwanza kutoka Afrika

Masuala ya UM

Dkt. Tulia Ackson kutoka nchini Tanzania amechaguliwa kuwa Rais mpya wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani IPU na mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo.

Uchaguzi huoumefanywa na Baraza la IPU linalojumuisha wabunge kutoka kote duniani na ambacho ndicho chombo kikuu kinachofanya maamuzi 

Dkt. Ackson anachukua nafasi kutoka kwa bwana Duarte Pacheco, mbunge kutoka Ureno, ambaye amehitimisha mamlaka yake ya miaka mitatu mwishoni mwa bunge la 147 la IPU mjini Luanda, Angola.

Wasifu wa Dkt. Tulia Ackosn

Dkt. Ackson alikua mbunge mwaka 2015. Kwa sasa ni spika wa bunge la Tanzania, nafasi ambayo aliteuliwa mwaka 2022 baada ya kuwa naibu spika kwa muda. 

Dkt. Ackson pia aliwahi kuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali mwaka 2015 Ana shahada ya kwanza na ya uzamili ya masuala ya sheria kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania na shahada ya uzamivu kutoka chuo kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini. 

Yeye ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na mwanachama wa Chama cha wanasheria Tanganyika. Bi Ackson pia alifundisha katika kitivo cha sheria cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya kuchaguliwa kwake hivi karibuni alizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu matarajio yake.

Nalikubali jukumu hili

Baada ya kuchaguliwa kwake Dkt. Ackosn amesema “Nashukuru kwa imani mliyonayo kwangu kwa kunichagua. Naikubali nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa huku nikitambua majukumu yote inayokuja nayo. Ninathibitisha tena kujitolea kwangu kufanya kazi bega kwa bega na ninyi nyote ili kuifanya IPU kuwa shirika lenye ufanisi zaidi, linalowajibika na lililo wazi zaidi.”

Wabunge walipiga kura ya siri. Kukiwa na wagombea wanne kwenye kura, Rais mpya wa IPU amechaguliwa kwa asilimia 57 ya kura baada ya duru moja ya upigaji kura.

Mamia ya wabunge kutoka wabunge 130 wanachama wa  IPU walipiga kura katika uchaguzi huo. 

Ili kuhimiza usawa wa kijinsia, kila Mbunge wa IPU alikuwa na haki ya kupata kura tatu kwa masharti kwamba wawe na wajumbe wenye uwiano wa kijinsia. Wajumbe wa jinsia moja walikuwa na haki ya kupata kura moja tu.

Historia imeandikwa

Kwa mara ya kwanza katika kihistoria, wagombea wengine watatu kwenye kura hiyo Bi. Adji Diarra Mergane Kanouté wa Senegal, Bi. Catherine Gotani Hara wa Malawi na Bi. Marwa Abdibashir Hagi wa Somalia wote walikuwa wabunge wanawake kutoka Afrika.

Bi. Ackson ni mwanamke wa tatu tu kuwa Rais wa IPU baada ya Najma Heptulla kutoka India (1999–2002) na Gabriela Cuevas kutoka Mexico (2017–2020). Pia ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kushika nafasi hiyo.

Baraza la uongozi la IPU huchagua Rais wa IPU kwa kipindi cha miaka mitatu. Rais wa IPU lazima awe mbunge kwa muda wote wa uongozi wake.

Rais ndiye mkuu wa kisiasa wa IPU, ambaye anaongoza mikutano yake ya kisheria na kuwakilisha shirika katika matukio ya kimataifa.

Kusoma zaidi bofya hapa.