Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani na usalama wa ulimwengu, mjadala muhimu kati ya Umoja wa Mabunge Duniani, IPU na UN

Dkt. Tulia Akson, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania.
UN News
Dkt. Tulia Akson, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania.

Amani na usalama wa ulimwengu, mjadala muhimu kati ya Umoja wa Mabunge Duniani, IPU na UN

Masuala ya UM

Februari 8 na 9 mwaka huu 2024, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani umefanyika mkutano wa pamoja kati ya Umoja wa Mabunge Duniani na Umoja wa Mataifa ambapo mkutano huu wa kila mwaka unaokutanisha uwakilishi wa mabunge kutoka kote duniani hujadili masuala kadha yanayohusu ulimwengu mzima na kuona namna ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuyafikia malengo ya kuifanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi.

Dkt. Tulia Akson, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania. Dkt. Tulia ni mmoja wa waliohudhuria mkutano huo.

Rais huyo wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson akihojiwa na Anold Kayanda wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa anasema kupitia mkutano huu wamepata nafasi ya kujadiliana mambo mengi lakini jambo kubwa likiwa usalama na amani ya ulimwengu.

« Mojawapo ya mambo ambayo tumekubaliana kwenye hili eneo ni kuweka nafasi ya pande mbili (zinazokinzana) kuzungumza. » Anaeleza Dkt. Tulia akiongeza pia kuwa wamejadili suala la matumizi ya teknolojia ya akili mnemba au Artificial Intelligence katika kuipeleka dunia kwenye maendeleo endelevu.

Kuhusu usalama na amani ya Dunia, alipoulizwa kuhusu mikakati yake kama kiongozi wa chombo hiki kikubwa cha mabunge 180 duniani, Dkt. Tulia anasema yeye anaamini katika ushirikishaji kwa hivyo ana mpango wa kuhakikisha ninazungumza na pande zinazokinzana, na “hata katika mkutano huu nimepata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya pande zinazosigana na tumekubaliana kwamba katika mkutano unaokuja mwezi Machi” watakuja na yale ambayo amewaomba kuyafanya ingawa hakutaka kuyataja kwani yako katika hatua inayosubiri utekelezaji na hapo ndipo anaweza kuamua hatua za kuchukua.

Kuhusu lengo namba tano la Umoja wa Mataifa la maendeleo endelevu linaloangazia usawa wa kijinsia, Rais huyo wa IPU anasema anao mkakati wa kutembelea nchi mbalimbali ambako uwakilishi wa wanawake hasa katika vyombo vya uwakilishi wa wananchi ni mdogo ili kuhamasisha na kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za kukaa kwenye meza ya maamuzi.

Wabunge ni wawakilishi wa wananchi  

Kuhusu mtazamamo wake dhidi ya wabunge kuegemea upande wa serikali badala ya kuwakilisha mawazo ya wananchi wanaowawakilisha, Dkt. Tulia ambaye kimsingi licha ya kuwa Rais wa IPU lakini ni Mpunge na pia Spika wa Bunge la Tanzania, misimamo wake ni kwamba wabunge wanaweza kuisifia serikali ikifanya vizuri, na pia ikiwa ni mawaziri ambao ni wabunge pia wanaweza kuitete serikali kwa nafasi zao, lakini kazi hasa ya mbunge wa kawaida ni kuwakilisha mawazo ya wananchi katika Bunge na si vinginevyo.