Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde twataka hatua kulinda wabunge wanaoteswa- IPU

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa mabunge duniani, IPU
IPU
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa mabunge duniani, IPU

Chonde chonde twataka hatua kulinda wabunge wanaoteswa- IPU

Haki za binadamu

Mkutano wa 140 wa Baraza la umoja wa mabunge duniani, IPU umelaani vikali mateso, vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu wa wabunge kote duniani.

Taarifa ya IPU iliyotolewa leo huko Doha, Qatar, kunakofanyika mkutano huo imesema hayo ikinukuu taarifa ya kamati ya  haki za binadamu za wabunge ya IPU ambayo ina haki za kipekee za kusaidia wabunge walio hatarini.

Kauli ya kamati hiyo inafuatia uchunguzi wake wa visa 187 kwenye nchi kadhaa ambamo kwazo haki za wabunge zinasigingwa.

Nchi zilizochunguzwa ni Uturuki, Venezuela, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Maldives, Ufilipino, Uganda, Cote d’Ivoire, Indonesia, Niger, Brazil, Ecuador na Mongolia.

Asilimia 84 ya wabunge hao ni kutoka upinzani ilhali asilimia 25 ni wanawake.

Venezuela

Nchini Venezuela, kamati imechunguza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wabunge 64 kutoka upande wa upinzani ambao wamekumbwa na ukamati holela, kuswekwa rumande bila kesi zao kusikilizwa na kuzuia kutekeleza majukumu yao ya kibunge.

Wabunge hao wanapinga serikali ya Rais Nicolas Maduro na licha ya kupata idadi kubwa ya viti bungeni kufuatia uchaguzi wa mwaka 2015,  bado hawajapatiwa fedha ili kufanikisha shughuli zao.

Katika tukio la hivi karibuni, wabunge wawili walizuia kwenye kiwanja cha ndege mjini Caracas, ili wasisafirikwenda Doha Qatar kushiriki mkutano wa IPU.

Uturuki

Zaidi ya mashtaka 600 ya uhalifu na ugaidi yanakabili wabunge 61 wa chama cha HDP tangu mwezi Disemba mwaka 2015 wakati katiba ilivyofanyiwa marekebisho ili kuondoka kinga dhidi ya wabunge wote.

Wabunge 10  hadi sasa wanashikiliwa korokoroni.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Angalau huko DRC, kuna nuru kwa kuwa wabunge wawili wa zamani waliokuwa wanashikiliwa kwa muda mrefu wameachiwa huru, kitendo kinachopongezwa na IPU.

Wabunge hao ni Franck Diongo na Eugène Diomi Ndongala ambapo tangu mwaka 2012, kamati ya IPU imekuwa ikisaka kuachiliwa huru kwa Ndongala na mwaka 2016 kwa Diongo.

Tangu mwezi Juni mwaka 2012, Bwana Ndongala amekuwa akilengwa na kampeni za kisiasa na kisheria ili kumuengua kwenye mchakato wa kisiasa ambapo hata hivyo IPU inalalama kuwa hajapatiwa msamaha wa rais kama ilivyo kwa wafungwa wengine wa kisiasa.

Diongo, ambaye alikamatwa mwezi Disemba mwaka 2016 na askari wa kundi la walinzi wa rais, yaripotiwa kuwa akiwa korokoroni aliteswa na kushtakiwa licha ya mazingira dhoofu ya afya yake. Hata hivyo yeye amepatiwa msamaha wa rais jambo ambalo IPU imepongeza.

Ufilipino

Nchini Ufilipino, IPU bado ina wasiwasi mkubwa kwa kuwa miaka miwili tangu kukamatwa, seneta Leila de Lima bado yuko korokoroni licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wowote wa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

IPU inatoa wito kwa mamlaka nchini humo zimwachie huru haraka na mchakato wowote wa kisheria dhidi yake utupiliwe mbali.

Umoja huo wa mabunge duniani unasema kuwa iwapo hilo halitafanyika, utaitisha msimamizi wake wa mashtaka aruhudiwe ili aweza kufuatilia uhalili wa mchakato wa kesi inayoendelea.