Mabunge thabiti ni msingi mkuu wa demokrasia na maendeleo

30 Juni 2019

Leo ni siku ya mabunge duniani ambapo Umoja wa Mataifa unaeleza umuhimu wa mabunge hayo katika kupaza sauti za wananchi.
 

Siku hii ni tarehe ambayo ulianzishwa Umoja wa mabunge duniani, IPU ambapo inaelezwa kuwa vyombo hivyo  pindi vinapokuwa thabiti ni msinigi wa demokrasia.

“Mabunge yanawasilisha sauti za wananchi, yanapitisha sheria, yanapanga mafungu ya fedha kwa ajili ya kutekeleza sheria na sera na pia huwajibisha serikali,” umesema Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika mabunge yanafanya kazi kuhakikisha sera zinanuafisha wananchi, hususan wale walio hatarini zaidi, kwa kupitisha sheria kama vile zile za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na kuhakikisha pia kuna huduma sawa za afya.

Mabunge pia yanaunganisha ajenda za kimataifa na za kitaifa kwa kuhakikisha kuwa serikali zinatekeleza mikataba ya kimataifa ambayo serikali hizo zimeridhia.

UN Photo/Eric Kanalstein
Wanawake wabunge Afghanistan wakiingia Bungeni (Wolesi Jirga )

Mathalani ajenda 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na IPU imekuwa ikishirikiana na mabunge kuona jinsi gani inaweza kujenga uwezo wa kufanikisha hoja hiyo.

Bunge la zamani zaidi liko Iceland na lilianzishwa mwaka 930.

“Katika nchi ambazo zimeibuka kutoka kwenye mizozo, mabunge thabiti yanaweza kusaidia kuwepo kwa mpito wenye amani kwa njia ya demokrasia kwa kuweka mazingira bora ya maridhiano na mashauriano,”  umesema Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa IPU, kila nchi duniani ina aina Fulani ya serikali wakilishi ambapo kuna aina mbili za mabunge yale yenye sehemu mbili ambayo ni bunge la juu na la chini na kuna mabunge yenye bunge moja tu.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya nchi 193, nchi 79 zina bunge la juu na la chini ilihali nchini 114 zina bunge moja tu na hivyo kufanya kwa ujumla kuna zaidi ya wabunge 46,000.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa bunge la zamani zaidi ni Althingi, la huko Iceland ambalo lilianzishwa mwaka 930.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud