Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: Vita na mizozo vyasababisha watu milioni 114 kuyakimbia makazi yao

Wahamiaji wakija ufukweni kutoka mto Chucunaque baada ya kuvuka msitu wa Darien.
© IOM/Gema Cortes
Wahamiaji wakija ufukweni kutoka mto Chucunaque baada ya kuvuka msitu wa Darien.

UNHCR: Vita na mizozo vyasababisha watu milioni 114 kuyakimbia makazi yao

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, mateso, ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu huenda ikazidi watu milioni 114 limesema Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Hayo yapo kwenye ripoti ya nusu mwaka wa 2023 ya UNHCR iliyotolewa hii leo huko Geneva Uswisi ambayo imechanganua mabadiliko na mienendo ya watu kulazimika kukimbia makazi yao katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo yam waka huu 2023 na kutoa takwimu za muhimu za wakimbizi wanaotafuta hifadhi, wakimbizi wa ndani, wakimbizini wasio nan chi zinazo wa hifadhi pamoja na nchi zao za asili.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi anasema Ingawa ulimwengu kwa sasa unafuatilia janga la kibinadamu huko Gaza. “Lakini duniani kote, migogoro mingi sana inaongezeka huku ikisambaratisha maisha ya watu wasio na hatia na kung’oa watu,” 

Vichochezi vikuu vilivyolazimisha watu kuyakimbia makazi yao ni pamoja na: vita nchini Ukraine na migogoro katika mataifa ya Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC na Myanmar, mchanganyiko wa ukame, mafuriko na ukosefu wa usalama nchini Somalia na mzozo wa muda mrefu wa kibinadamu nchini Afghanistan.

Grandi ameeleza haja ya jumuiya ya kimataifa kushughulikia tatizo hili "Kutoweza kwa jumuiya ya kimataifa kusuluhisha mizozo au kuzuia mizozo mipya kunasababisha watu kuhama na huzuni, Ni lazima tuangalie ndani, tushirikiane kumaliza mizozo na kuruhusu wakimbizi na watu wengine waliokimbia makazi yao kurejea nyumbani au kuanza upya maisha yao.”

Takwimu

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022 watu milioni 1.6 walikimbia makazi yao na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Juni, watu milioni 110 walikuwa wamekimbia makazi yao ulimwenguni kote.

 Zaidi ya nusu ya watu wote ambao wanalazimika kukimbia hawavuka mpaka wa kimataifa, katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Juni hadi mwisho wa  mwezi Septemba, UNHCR inakadiria kuwa idadi ya waliolazimika kuyakimbia makazi yao iliongezeka kwa milioni 4, na kufikisha jumla ya watu milioni 114.

Mzozo wa Mashariki ya Kati uliozuka tarehe 7 Oktoba 2023, upo nje ya muda ulioangaziwa ripoti hii hivyo hivyo matokeo yake hayakuwekwa katika ripoti hii.

"Tunapotazama matukio yanayoendelea Gaza, Sudan na kwingineko, matarajio ya amani na suluhu kwa wakimbizi na watu wengine waliokimbia makazi yao yanaweza kuhisi kuwa mbali, lakini hatuwezi kukata tamaa. Pamoja na washirika wetu tutaendelea kusukuma mbele - na kutafuta - suluhu kwa wakimbizi." Alisema, Grandi.

Wakimbizi wengi kutoka nchi za kipato cha chini  na kati

Asilimia 75 ya wakimbizi na watu wengine wanaohitaji ulinzi wa kimataifa, Ulimwenguni, wanatoka katika mataifa ya kipato cha chini na cha kati. 

Mpaka sasa UNHCR wamesema wamepokea maombi mapya milioni 1.6 ya kusaka hifadhi ya watu binafsi katika miezi sita ya kwanza, idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.

Zaidi ya wakimbizi 404,000 waliorejea walirekodiwa, idadai hii ni zaidi ya mara mbili ya kipindi kama hicho mwaka 2022, ingawa wengi hawakuwa katika hali salama.

Takriban wakimbizi wa ndani milioni 2.7 walirejea nyumbani katika kipindi hicho, zaidi ya mara mbili ya waliorejea katika nusu ya kwanza ya 2022, idadi ya wakimbizi waliopewa makazi mapya iliongezeka.

Ripoti hiyo itazinduliwa katika kipindi cha pili cha Jukwaa la Wakimbizi Duniani (GRF), mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa wakimbizi na watu wengine waliolazimika kuyakimbia makazi yao na utafanyika jijini Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 13 hadi 15 mwezi Disemba. 

Serikali, wakimbizi, mamlaka za mitaa, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia na sekta binafsi watakusanyika pamoja katika mkutano huo ili kuimarisha mwitikio wa kimataifa na kutafuta suluhu kwa changamoto ya watu kuyakimbia makazi yao.