Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Kenya kwa kuamua kuwapatia uraia wenye asili ya Rwanda na Zimbabwe- UNHCR 

Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.
UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto wa umri wa miezi mbili apokea cheti cha kuzaliwa mjini Accra,Ghana.

Heko Kenya kwa kuamua kuwapatia uraia wenye asili ya Rwanda na Zimbabwe- UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limekaribisha uamuzi wa serikali ya Kenya wa kuwapatia utaifa  jumla ya watu 2,970 ambao awali hawakuwa na utaifa wowote na hivyo kushindwa kupata huduma za msingi ikiwemo elimu, afya na ajira. 

Rais Uhuru Kenyatta alitoa uamuzi huo mwishoni mwa wiki ambao unahusisha watu 1,670 wa jamii ya kishona kutoka Zimbabwe na 1,300  kutoka Rwanda ambapo sasa wanakuwa raia wa Kenya. 

Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya Fathiaa Abdalla amenukuliwa akisema “haya ni maendeleo makubwa ya kuleta mabadiliko kwa maelfu ya watu. Tunapongeza uamuzi wa serikali ya Kenya wa kuwapatia uraia, kuhakikisha kuwa wanajumuishwa kikamilifu kwenye jamii. Hii pia inafungua njia kwa mataifa mengine kufuata mfano pindi linapokuja suala la kutatua hali ya watu kutokuwa na utaifa kwa muda mrefu.” 

Jamii ya washona iliwasili Kenya miaka ya 1960 kutoka Zimbabwe wakati huo ikijulikana Rhodesia Kusini na kisha Rhodesia wakiwa wamisionari wa dini ya kikristo. 

Washona hao waliwasili wakiwa na hati za kusafiria za Uingereza na kusajiliwa kama vijakazi wa Uingereza. 

Hata hivyo mara baada ya uhuru wa Kenya mwaka 1963, walikuwa na kipindi cha miaka mwili tu ya kujiandikisha kuwa raia wa Kenya, fursa ambayo waliikosa. 

Halikadhalika kwa kuwa walikuwa hawaiishi tena kwenye nchi ambamo walikuwa wanaishi walipozaliwa, walijikuta hawana utaifa. 

Kwa upande wa wanyarwanda, wengi wao walikwenda nchini Kenya miak aya 1930 kufanya kazi kwenye mashamba ya chai katika kaunti ya Kericho. 

Kutokana na masuala kadhaa ikiwemo yale yanayofanana na washona, wanyarwanda hao walijikuta hawana utaifa. 

“kutambuliwa kuwa ni raia, kunatoa hakikisho la kupata haki zao za msingi kama vile elimu, afya, ajira, kumiliki mali na huduma za kifedha,” amesema mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya. 

Uamuzi huu wa serikali ya Kenya unafuatia ahadi ambayo serikali hiyo ilitoa kwa UNHCR wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na UNHCR kuhusu ukosefu wa utaifa mwezi Oktoba mwaka 2019. 

Katika kikao hicho, Kenya iliahidi kuridhia mkataba wa kimataifa kuhusu ukosefu wa utaifa. 

Nchini Kenya kunakadiriwa kuwepo kwa watu 18,500 wasio na utaifa na wengi wao wanatoka jamii za makabila madogo. 

Kando mwa washona na wanyarwa, kuna watu wa jamii ambayo wazee wao walitoka kisiwani Pemba Tanzania. 

UNHCR imesema kwa kuzingatia kampeni ya #IBelong ya kutokomeza ukosefu wa utaifa, itaendelea kusaidia juhudi za Kenya za kutatua na kumaliza suala la watu kukosa utaifa nchini humo.