Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukosa cheti cha kuzaliwa ni sawa na mnyama aliye mwituni- Damas

Damas Ngolo, mtu asiye na utaifa ambaye anatoka jamii  ya watu wa asili nchini Jamhuri ya Congo.
UNHCR Video
Damas Ngolo, mtu asiye na utaifa ambaye anatoka jamii ya watu wa asili nchini Jamhuri ya Congo.

Kukosa cheti cha kuzaliwa ni sawa na mnyama aliye mwituni- Damas

Haki za binadamu

Zaidi ya watu 25,000 wa jamii ya asili nchini Jamhuri ya Congo wako hatarini kukosa utaifa. Wengi wao hawana nyaraka kama vile vyeti vya kuzaliwa na wanaishi katika maisha ya ufukara katika maeneo ya ndani zaidi ya nchi hiyo.
 

 

Soundcloud

Miongoni mwao ni Damas Ngolo ambaye hata hatambui umri wake, yeye mwenyewe hajawahi kwenda shule na anasema, “watu wanaoishi bila nyaraka, ni kama wanyama watembeao msituni.”

Mwanakijiji huyu anaitoa kauli hii akiwa ameketi nje ya nyumba yao iliyojengwa kwa udongo na nyasi akienda mbali zaidi akitambulisha familia yake akisema “mke wangu anaitwa Marie Ngo Nkoli na mimi naitwa Ngolo Damas.”

Damas na familia yake ni miongoni mwa takribani watu wa jamii ya asili Elfu 25 katika Jamhuri ya Congo au Congo-Brazaville walio hatarini ya kutokuwa na utaifa kwa sababu hawana nyaraka zozote za kuthibitisha utaifa wao kwa hiyo ni sawa na kwamba hawaishi.

Yeye ana watoto sita, wa kike watatu na wavulana watatu. Watoto wake hawajawahi kuwa na vyeti vya kuzaliwa. Walianza kwenda shuleni bila nyaraka zinazotakiwa na ndipo walizuiwa kuendelea na  masomo. 
Sasa watoto wanasalia nyumbani wakitengeneza mitego ya  ndege na kwenda msituni kuwinda.

Damas Ngolo na familia yake kutoka Jamhuri ya Congo. Hawana Utaifa na wanatoka jamii ya watu wa asili.
UNHCR Video
Damas Ngolo na familia yake kutoka Jamhuri ya Congo. Hawana Utaifa na wanatoka jamii ya watu wa asili.

Ukiwa huna cheti cha kuzaliwa, elimu na afya ni ndoto

UNHCR inasema idadi kubwa ya watu wa jamii ya asili wasio na vyeti wanaishi kifukara na wanahaha kukimu mahitaji yao. Hawawezi kwenda shuleni, kuajiriwa au kupata huduma za msingi.

Tiba Cyr Maixent ni mshauri kutoka Wizara ya haki za binadamu na uendelezaji wa watu wa asili Congo Brazaville na anasema, “Wengi wao hawana vyeti vya kuzaliwa na hawana nyaraka za kuonesha hadhi ya uraia wao. Watu hawa wa asili ni miongoni mwa wanajamii ya Congo lakini ni jamii yenye shida nyingi. Kwa muda mrefu wamekuwa wanaenguliwa."

Sensa ya watu iliyofanyika Congo Brazaville miaka mitatu iliyopita ilibainisha kuwepo kwa watu milioni 5.8 nchini humo ambapo kati yao hao 199,440 hawana vyeti vya kuzaliwa na miongoni mwao ni watu wa asili 25,000.
Takwimu hizo zilisababisha serikali kwa kushirikiana na UNHCR kuanzisha kampeni ya usajili wa vizazi ili kupatia watu wa asili vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni sawa na kibali cha uhai mpya.

Kwa Damas akionekana na mawazo anasema "nilizaliwa kijiji cha Ebala. Nilikuja hapa Vono nikiwa mtoto. Wakati mwingine naenda msituni na kukusanya mboga mboga. Tunapata kiasi kidogo tu kwa ajili ya chakula, hakuna ziada ya kuuza na ndio maana hatuna fedha hata ya kununulia nguo.”

Mavazi yake na familia yake ni kuukuu. Kando ya mavazi, mlo nao ni shida akisema “hatuna chakula cha kutosha, hatuna chochote, tunataabika sana.”

UNHCR inasema Damas na wenzake ni sehemu ya mamilioni ya watu duniani wasio na utaifa na hawana nyaraka za kuthibitisha utaifa wao na hivyo kukosa huduma kama elimu, ajira na afya.

Quentin Banga, mtaalamu wa UNHCR kuhusu ukosefu wa utaifa anasema “unahitaji nyaraka ili kuondokana na ukosefu wa utaifa, suala ambalo hii leo linatambuliwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”

Kampeni ya IBelong yaanza kuzaa matunda

Ndio maana UNHCR kuanzia mwaka 2014 ilianza kampeni ya IBelong au MiminiWa kwa lengo la kupatia watu haki yao ya msingi ya cheti cha kuzaliwa. Hadi leo takribani watu 5,000 wa jamii ya asili wamepatiwa vyeti na wengi zaidi wanafikiwa kama Mawaki Ngandibi wa kijiji cha Vono.

Mawaki mwenye umri wa miaka 24 akiwa nyumbani kwake hakuamini furaha yake kuwa familia yake inanufaika na mpango wa UNHCR. Mwezi Septemba yeye na mkewe Nadine walipokea cheti cha kuzaliwa cha mtoto wao Doudé  mwenye umri wa miezi 18. Hafla ya utoaji vyeti ilifanyika mj iwa Djambala na sasa anasema, “Ninafurahia sana cheti cha kuzaliwa cha mtoto wangu kwa sababu akikua nitaweza kumpeleka shuleni. Kwa kuwa amepatiwa cheti sasa atafahamu kuwa baba yake ninaweza kumwandikisha shule.”

Kwa Damas na mkewe Maria, walishawasilisha nyaraka zao na wanatumai kuwa watapata pia vitambulisho vyao ili kuondokana na adha ya kushindwa kuandaa mustakabali wa watoto wao.