Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Israel na Palestina huku mzozo wa Gaza ukizidi kuwa mbaya

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakutana kujadili mzozo wa Gaza.
UN Photo/Eskinder Debebe
Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakutana kujadili mzozo wa Gaza.

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Israel na Palestina huku mzozo wa Gaza ukizidi kuwa mbaya

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani katika mkutano wake wa kila robo mwaka kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Israel na Palestina, ambao sasa unapewa uharaka zaidi kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas tarehe 7 Oktoba na kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano huo amesema “hali inazidi kuwa mbaya kila saa”, na kurejea wito wake wa kusitisha mapigano mara moja. 

Baraza la Usalama likisikiliza maelezo ya Bi. Lynn Hastings (Kwenye skrini), Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.
UN Photo/Eskinder Debebe
Baraza la Usalama likisikiliza maelezo ya Bi. Lynn Hastings (Kwenye skrini), Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

'Ubinadamu unaweza kushinda'

Akitoa taarifa kwa Baraza hilo, Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, Lynn Hastings, amesema makubaliano ya kurejesha misaada kupitia mpaka wa Rafah nchini Misri, na kuachiliwa kwa idadi ndogo ya mateka katika siku chache zilizopita “inaonesha kuwa kupitia diplomasia na mazungumzo, ubinadamu unaweza kutawala, na tunaweza kupata suluhu za kibinadamu, hata katika kina kirefu cha migogoro”. 

Ulimwengu unatazamia Nchi Wanachama wa Baraza hili kutekeleza sehemu yake - Lynn Hastings

Amezitaka nchi zote zenye ushawishi kutekeleza hilo na kuhakikisha kuna kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, alisema raia lazima wawe na mahitaji muhimu ya kuweza kuwasaidia kuishi. Kwa hivyo, upitishaji wa misaada kwa haraka wa misaada ya kibinadamu lazima iwezeshwe, na watu waunganishiwe tena maji na umeme.

Alitua salamu za rambirambi kwa wafanyakazi wenzake 35 wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya Palestina (UNRWA) ambao wameuawa wakati wa mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza.

Wahusika wa pande zote “lazima kuchukua tahadhari mara kwa mara, kuwaokoa raia”, na wakati huduma za maji na umeme zikirejeshwa tena, kwa mujibu wa sheria za vita.

“Ikiwa tunataka kupunguza janga hili la kibinadamu, mazungumzo lazima yaendelee - ili kuhakikisha mahitaji muhimu vinaweza kuingia Gaza kwa kiwango kinachohitajika, kuwaokoa raia na miundombinu wanayoitegemea, kuwaachilia mateka, na kuepuka ongezeko lolote zaidi,” alisema na kuongeza kuwa “Ulimwengu unatazamia Nchi Wanachama katika Baraza hili kushika sehemu yake katika kuongoza njia.”

Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta maji huko Gaza.
© WHO/Ahmed Zakot
Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta maji huko Gaza.

'Vigingi vimeongezeka Maradufu': Wennesland

Akizungumzia hatari ya sasa ya mzozo kuenea katika eneo kubwa zaidi, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, Tor Wennesland, amesema yeye na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakitafuta "nafasi yoyote" kushughulikia hali hiyo mashinani na kuzuia vifo na masaibu zaidi kwa raia.

"Ni muhimu, kwamba sisi, kama jumuiya ya kimataifa iliyoungana, tutumie juhudi zetu zote za pamoja kukomesha umwagaji damu na kuzuia kuenea zaidi kwa uhasama, ikiwa ni pamoja na katika Ukanda,” Ameongeza kuwa “Vigingi vimeongezeka maradufu, na ninatoa wito kwa watendaji wote wanaohusika kuchukua hatua kwa uwajibikaji."

Ameonya kuwa maamuzi yoyote yatakayofanyika bila ya kupigiwa hesabu vizuri yataweza kuwa na "matokeo yasiyopimika", akiongeza kuwa matukio haya mabaya hayajaachana na muktadha mpana katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina, Israel, na ukanda wote huo.

Kwa kizazi kizima, matumaini yamepotea, alisisitiza.

“Ni suluhu ya kisiasa pekee ndiyo itakayotusogeza mbele,” alisema. “Hatua tunazochukua kukabiliana na mzozo huu lazima zitekelezwe kwa njia ambayo hatimaye itaendeleza amani iliyojadiliwa ambayo inatimiza matarajio halali ya kitaifa ya Wapalestina na Waisraeli - maono ya muda mrefu ya Nchi mbili, kulingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na makubaliano ya awali.”

Katibu Mkuu António Guterres ahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu António Guterres ahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.

'Kila saa hali inazidi kuwa mbaya zaidi': Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa kile alichokiita utangulizi wa mgogoro wa sasa, akisema hali katika Mashariki ya Kati "Hali inazidi kuwa mbaya kila baada ya saa".

"Migawanyiko inasambaratisha jamii na mivutano inatishia kuchanganya zaidi.", alisema.

"Ni muhimu kuwa wazi juu ya kanuni," aliongeza, kwa kuanza na ulinzi wa raia.

Katibu Mkuu Guterres alisisitiza haja ya kusitisha mapigano mara moja kwa sababu za kibinadamu, “kupunguza mateso makubwa, kufanya utoaji wa misaada kuwa rahisi na salama na kuwezesha kuachiliwa kwa mateka”.

Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen akiwa ameshikilia picha ya wale waliotekwa nyara na Hamas, amesema hali ya mateka ni jinamizi lililo hai. Amekumbusha shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israeli, akisema siku hiyo "itaingia katika historia kama mauaji ya kikatili na kengele ya kutuamsha dhidi ya itikadi kali na ugaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Palestina.
UN Photo/Manuel Elías
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Palestina.

"Hamas ndio Manazi wapya," amesema, akitoa wito wa "kuachiliwa mara moja kwa mateka wote na bila masharti yoyote. “

Na kisha aakamuuliza Katibu Mkuu unaishi katika dunia ipi? Kwa hakika sio dunia hii.

Akizungumzia uwezekano wa Qatar kusaidia waziri huyo ameiambia Jumuiya ya Kimataifa kwamba "Ninyi, wanachama wa jumuiya ya kimataifa, mnapaswa kuitaka Qatar kufanya hivyo. Mkutano unapaswa kumalizika kwa ujumbe bayana warejesheni nyumbani."

Israel ina haki na wajibu wa kujilinda, amesema. "Sio vita vya Israeli pekee. Ni vita vya ulimwengu huru."

Hatua dhidi ya mauaji ya Oktoba 7 ni suala la kujilinda amesema, akiyashukuru mataifa kwa kuunga mkono Israeli.

Waziri huyo wa mambo ya nje ameendelea kusema kwamba “Tutashinda kwa sababu vita hii ni ya Maisha, vita hii lazima iwe vita yako pia. Hivi sasa, ulimwengu unakabiliwa na chaguo la wazi la maadili".

Ameongeza kuwa "Mtu anaweza kuwa sehemu ya ulimwengu uliostaarabika au kuzungukwa na uovu na ukatili, huwezi kuwa katikati."

Amemalizia kwa kusema kwamba “Iwapo mataifa yote hayatasimama kidete na dhamira ya Israel ya kuondoa magaidi kutoka kwenye uso wa dunia, huu utakuwa wakati wa giza totoro kwa Umoja wa Mataifa ambao hautakuwa na uhalali wa kimaadili wa kuwepo".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi ya Palestina Riad Al-Malki akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.
UN Photo/Eskinder Debebe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi ya Palestina Riad Al-Malki akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.

Palestina

Riyad al-Maliki Waziri wa mambo ya nje wa Palestina alisema Baraza la Usalama na jumuiya ya kimataifa ina wajibu na jukumu la kuokoa maisha.

Ameongeza kuwa "Kuendelea kushindwa katika Baraza hili la Usalama hakuna udhuru”.

Amesisitiza kuwa ni "Sheria na amani ya kimataifa pekee ndizo zinazostahiki kuungwa mkono n anchi zote bila masharti akiongeza kwamba ukiukwaji zaidi wa haki na mauaji zaidi , havitafanya Israeli kuwa salama."

Pia amesema "Hakuna kiasi cha silaha, wala hakuna muungano, utakaoiletea usalama ni amani tu, amani na Palestina na watu wake. Hatma ya watu wa Palestina haiwezi kuendelea kunyang'anywa, kufukuzwa, kunyimwa haki na vifo. Uhuru wetu ni hali ya kugawana amani na usalama.”

Bwana al-Maliki amesisitiza kwamba kuepuka maafa makubwa zaidi ya kibinadamu na kusambaa katika maeneo mengine "lazima iwe wazi kwamba hii inaweza tu kufikiwa kwa kukomesha mara moja vita vya Israel vilivyoanzishwa dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza. Kukomesha umwagaji damu.