Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya wiki ya utulivu hofu na mashambulizi vyarejea tena Gaza: UN

Mwanamume Mpalestina akiwabeba watoto wawili wadogo kupitia eneo lenye vifusi huko Gaza wakati wa mapumziko ya kibinadamu.
© UNRWA/Ashraf Amra Mwanamume akiwapeleka watoto wake kuelekea eneo salama wakipitia katika ardhi iliyolipuliwa kwa bomu katika Ukanda wa Gaza wakati wa usitishaji vita kwa ajili ya kufikisha msaada wa kibinadamu. (Maktaba)

Baada ya wiki ya utulivu hofu na mashambulizi vyarejea tena Gaza: UN

Amani na Usalama

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumzia masikitiko yake makubwa kuhusu kuanza tena kwa operesheni za kijeshi huko Gaza leo, wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameahidi kusalia na kusaidia wale wote wanaohitaji msaada, huku wakisisitiza "hakuna mahali popote palipo salama kutokana na mashambulizi" katika eneo la Gaza lililoharibiwa na vita.

Milio ya makombora na milipuko ilishamiri muda mfupi baada ya saa 7 asubuhi kwa saa za Gaza na ilisikika waziwazi katika hospitali ya Nasser Kusini mwa mji huo ambapo watoto wenye hofu na kiwewe mara moja waliwang'ang'ania mama zao kwa hofu, amesema James Elder kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.

Bwana Elder amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kupitia njia ya video kutoka Khan Younis Gaza, kabla ya kulaani kuendelea kwa athari za vita hiyo kwa watoto akisema "Mabomu yalianza sekunde chache tu baada ya muda wa kusitishwa kwa mapigano kumalizika, hii ni zahma kubwa inavyoendelea dhidi ya watoto".

Wapalestina, wakiwemo watoto na wanawake, wanaonekana wakisafiri na mali zao nyuma ya lori wakati wa mapumziko ya muda ya kibinadamu huko Gaza.
© UNRWA/Ashraf Amra Wakaazi wa Gaza wakihamisha mali zao wakati wa sitisho la vita wa muda kwa ajili ya haki za kibinadamu.

Majeraha ya vita

Bwana Elder amesema "Tulipokaribia hospitali ya Nasser kulikuwa na mlipuko, kombora, roketi, kitu kilitokea. Watoto wenye majeraha ya vita wako kila mahali, watoto wenye majeraha ya vita bado wako kwenye shoroba. Mamia ya wanawake na watoto hukimbilia humu. Unatoka chumba cha wagonjwa mahuututi au ICU na kuna familia za watu watano inajibana kwenye godoro linalotosha watu wawili."

Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya kibinadamu kurejea kwa ghasia kunafuatia kumalizika kwa muda wa wiki moja wa usitishwaji uhasama kati ya wanamgambo wa Hamas na wanajeshi wa Israel ambao uliruhusu kufikishwa kwa mafuta, chakula na maji yanayohitajika sana, ambayo watu wamekuwa wakiyanywa mara tu yanapopewa, 

Kusitishwa huko kwa mapigano pia kuliwezesha kuachiliwa kwa mateka waliochukuliwa wakati wa shambulio la ghafla la Hamas la Oktoba 7 kusini mwa Israel na kusababisha mauaji ya takriban watu 1,200, na pia kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina waliokuwa wanashikiliwa nchini Israel.

Mamlaka ya afya ya Gaza imeripoti vifo vya zaidi ya watu 15,000 tangu mashambulizi ya Israel kuanza, huku maelfu ya watoto wakiaminika kufukiwa chini ya vifusi. 

Mgogoro huo pia umesababisha ulemavu wa viungo kwa takriban watoto 1,000 katika wiki za hivi karibuni, amebainisha bwana Elder.

Mkuu wa UN aongoza ombi jipya la kusitisha mapigano

Kupitia ukurasa wake wa X, ambayo zamani ilikuwa  Twitter, Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres anaongoza wito wa pande zinazozozana kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kukubaliana juu ya usitishaji vita wa muda mrefu kuweza kuruhusu misaada inayohitajika sana kuingia Gaza.

"Nasikitika sana kwamba operesheni za kijeshi zimeanza tena Gaza. Bado ninatumai kuwa itawezekana kufanya upya usitishaji mapigano ambao ulianzishwa. Kurejea kwa uhasama kunaonyesha tu jinsi ilivyo muhimu kuwa na usitishaji vita wa kweli wa kibinadamu."

Wanaume wakitembea kwenye vifusi na uchafu kutoka kwa majengo yaliyoharibiwa katika Jiji la Gaza, Oktoba 2023.
© WHO Wanaume wanatembea katika mitaa iliyoharibiwa ya Gaza.

Hebu tusaidie anahimiza mkuu wa OHCHR

Akitoa wito huohuo wa amani, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, ameonyesha wasiwasi wake mkubwa kutokana na matamko ya viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Israel "yanayopanga kupanua wigo na kuzidisha mashambulizi ya kijeshi".

"Kurejeshwa kwa vita huko Gaza ni janga," amesema mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa kabla ya kuzitaka pande zote na mataifa yenye ushawishi kwa pande zinazokinzana "kuongeza juhudi, mara moja, ili kuhakikisha usitishwaji wa mapigano  kwa misingi ya kibinadamu na haki za binadamu".

"Heshima kamili na ulinzi wa haki za binadamu za Wapalestina na Waisraeli bado ni muhimu sana, Bwana Türk amesisitiza, kabla ya kutoa wito wa kukomesha mara moja kwa ghasia na kuachiliwa kwa haraka na bila masharti kwa mateka wote waliosalia.

Ameongeza kuwa raia lazima walindwe kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu, akiiomba Israel "kama mamlaka inayokalia  kuhakikisha kwamba mahitaji ya kimsingi ya wakazi wa Gaza, kama vile chakula, maji, na matibabu, yanafikiwa. 

Amesisitiza kuwa “Ninazikumbusha pande zote wajibu wao wa kuruhusu na kuwezesha upitaji wa haraka na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa raia wanaohitaji, kote Gaza.”

Hospitali ni kama sinema ya kutisha

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limeonya kuwa mahitaji ya kimatibabu yanaendelea kuwa makubwa zaidi, huku kukiwa na vitanda 5,000 lakini vitanda 1,500 pekee na ni vituo 51 tu kati ya 72 ndivyo vinavyofanya kazi, amesema Dkt. Richard Peeperkorn, wa WHO ambaye ni mwakilishi wa shirika hilo katika eneo la Palestina linalokaliwa akizungumza kutoka Gaza.

Ameongeza kuwa "Mfumo wa afya wa Gaza umelemazwa na uhasama unaoendelea na ninataka kusisitiza kwamba hatuwezi kumudu kupoteza hospitali au vitanda zaidi."

Pia ameangazia utafiti katika jarida lakitabibu la The Lancet la Uingereza ambao umethibitisha takwimu za vifo zilizoripotiwa na mamlaka ya afya ya Gaza zikionyesha zaidi ya watoto 6,200 wamekufa, zaidi ya wanawake 4,000 na takriban wanaume 4,850, na zaidi ya watu 36,000 wamejeruhiwa.

Ambulensi iliyoharibika yenye herufi za Kiarabu na Kiingereza imesimama kwenye barabara iliyotengenezwa kwa lami huko Gaza. Mvulana mdogo amesimama kushoto, akiangalia gari, ambalo linaonyesha dalili za uharibifu mkubwa.
© UNICEF/Abed Zaqout Magari za kusafirisha majeruhi kwa dharura katika hospitali ya Al-Nasser huko Khan Younis yaharibiwa kufuatia shambulio la kombora mwanzoni mwa mzozo. (Maktaba)

Sakafu imejaa damu

Katika hospitali moja ndogo katika Jiji la Gaza ambacho ndicho kituo pekee cha watu waliojeruhiwa kinachofanya kazi kaskazini mwa eneo hilo, wafanyakazi wamezidiwa na "miili imepangwa kwenye maegesho ya magari nje na sakafu imejawa na damu," amesema Rob. Holden, Afisa Mwandamizi wa Dharura wa WHO.

Ameendelea kusema kuwa "Njia pekee ya kuielezea, hali hiyo ni kama sinema ya kutisha. Unapoingia ndani kuna wagonjwa kwenye sakafu walio na majeraha ya kiwewe ambayo unaweza kufikiria tu. Unajua, wagonjwa wanapewa huduma bora zaidi, lakini idadi ya wafanyikazi inayopatikana ni ndogo, na hao wachache waliopo wamekimbia na familia zao au wameuawa.”

Pia amesema "Vifaa havitoshi. Kumekuwa na matatizo makubwa ya kupata vifaa kaskazini mwa Gaza vilevile. Unapoingia hospitalini, unakutana na miili ya marehemu ambao wamefariki dunia walipowasili hospitalini au walipokuwa hospitalini, wakiwa wamepangwa nje wakisubiri ndugu wa familia waje kuwatambua.”

Akizungumza kutoka Gaza, afisa huyo wa WHO ameeleza kuwa madaktari, wauguzi, mafundi wa maabara na wahandisi "wanaofanya mitambo ifanye kazi, jenereta zinafanya kazi" walikuwa wakifanya kazi kwa siku za saa 22 "ili tu kuhakikisha kiwango cha msingi cha huduma".