Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi yakiendelea watoto 10,000 watapoteza maisha mwaka huu nchini Sudan: UN

Akina mama waleta watoto wao kwa uchunguzi wa lishe katika kliniki tembezi ya afya katika jimbo la Kassala, Sudan.
© UNICEF/Osman
Akina mama waleta watoto wao kwa uchunguzi wa lishe katika kliniki tembezi ya afya katika jimbo la Kassala, Sudan.

Mashambulizi yakiendelea watoto 10,000 watapoteza maisha mwaka huu nchini Sudan: UN

Msaada wa Kibinadamu

Ikiwa ni miezi sita tangu kuanza kwa machafuko nchini Sudan mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya duniani WHO na linalohusika na watoto UNICEF wameonya kuwa iwapo mashambulizi zaidi yataendelea na kukatizwa kwa huduma za afya na lishe kunaweza kugharimu zaidi ya maisha ya watoto 10,000 ifikapo mwisho wa 2023.

Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo kutoka Port Sudan nchini Sudan imeeleza kuwa tangu kuzuka kwa mapigano tarehe 15 Aprili 2023 watoto wamekuwa katika hatari za kupata kipindupindu, kidingapopo, surua, Malaria na magonjwa mengine bila ya kuwa na uwezo wa kutosha wa kuzuia na kwamba kuna hatari ya vifo kuongezeka ambavyo vingeweza kuzuilika. 

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Dkt Nima Saeed Abid amesema huduma za kimsingi za afya haziwezi kuwafikia mamilioni ya watu wenye uhitaji. 

“Wadau wetu wa afya wako tayari kwa dhamira kamili ya kutoa huduma za kuokoa maisha na kuzuia maisha ya watu kupotea kutokana na magonjwa yanayozuilika na kutibika. Wakati ni sasa wa kukomesha mashambulizi dhidi ya huduma za afya, kuhakikisha kuna ufikiaji salama na usiozuiliwa wa watoa huduma, kuna uendeshaji wa vituo vya afya kwa usalama pamoja na uwepo wa rasilimali za kutosha. Hata hivyo hatima yayote haya ni kupatikana amani, amani ndiyo jibu.”

Mamilioni ya familia wamenaswa katikati ya mapigano hayo, na zaidi ya watu milioni 5.8, ambao kati yao milioni 2.5 ni watoto, wamekimbia kusaka hifadhi sehemu nyingine.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, Mandeep O'Brien amesema utoaji wa huduma za afya ya mama, watoto wachanga na lishe kwa watoto ni huduma za kuokoa maisha nchini Sudan ambapo takriban watoto milioni 14 wanahitaji haraka lakini huduma hiyo imepungua katika baadhi ya maeneo pamoja na changamoto nyingine lukuki.

“Wafanyakazi wa afya hawajalipwa kwa miezi kadhaa. Ugavi umepungua. Miundombinu muhimu bado inashambuliwa. Mapigano yanahitaji kukomesha sasa, idadi ya vifo vya watoto haikubaliki. “ ameongeza O’Brien huku akisisitiza kuwa washirika wa afya wanahitaji kwa dharura upatikanaji na rasilimali kusaidia Sudan kuokoa afya na ustawi wa raia wake wachanga zaidi.

Takriban asilimia 70 ya hospitali katika majimbo yaliyoathiriwa na migogoro hazifanyi kazi. WHO imethibitisha mashambulizi 58 dhidi ya vituo vya kutolea huduma za afya hadi sasa, na vifo 31 pamoja na majeruhi 38 ambao ni wahudumu wa afya na wagonjwa.

Pamoja na changamoto za afya pamoja na mapigano makali yanayoendelea Khartoum, Darfur na Kordofans, msimu wa mvua unapunguza urahisi wa kuzifikia jumuiya zilizo katika mazingira magumu, huku mvua hizo zikihofiwa kuchochea kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na maji na vijidudu.