Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake, watoto na wazee ndio walioathirika zaidi na machafuko ya Upper Nile:Nyati

UNMISS imewasaidia wahudumu wa kibinadamu kuwahamisha maelfu ya watu waliotawanywa na vita Sudan Kusini
UNMISS / Eric Kanalstein
UNMISS imewasaidia wahudumu wa kibinadamu kuwahamisha maelfu ya watu waliotawanywa na vita Sudan Kusini

Wanawake, watoto na wazee ndio walioathirika zaidi na machafuko ya Upper Nile:Nyati

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya dharura OCHA nchini Sudan Kusini Bi. Sara Beysolow Nyanti awatembelea waathirika wa machafuko ya hivi karibuni kwenye maeneo ya  Adediang na Malakal, katika jimbo la Upper Nile State na kushuhudia madhila yanayowakabili .

Katika kitongoji cha Tonga hali ni dhahiri ya watu waliotawanywa na mapigano makali yaliyozuka baina ya vikundi vyenye silaha vya kitongoji hiki maeneo jiraji ya kaunti ya Panyikang na kuwalazimisha maelfu ya watu wasiojiweza wengi wakiwa wanawake, wazee na watoto kufungasha virago kwenda kusaka usalama wakiacha kila kitu na kuishia kwenye makambi haya.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu Sudan Kusini Sara Beyssolow Nyati na ujumbe wake wakiambatana na mamlaka ya eneo hili wamefika kuwatembelea waathirika hawa na kuzungumza nao ikiwa ni pamoja na jamii zinazowahifadhi ambapo wanawake, wazee na vijana walioathirika walipata fursa ya kueleza changamoto zao za kukimbia usiku wa manane na kutenganishwa na familia zao.

Na baada ya kuwasikiliza Bi.Sara akafunguka “Tunaweza kufanya kitu kwa wale waliotenganishwa na wapendwa wao wanaoishi sehemu nyingine, tutajaribu kadri tuwezavyo, tuko na wenzetu ambao wanafanyakazi kwa pamoja ili kuangalia jinsi gani tunaweza kuanza kuwafuatilia watoto na kuwaunganisha tena na mama zao, hata kuna watoto wengine wapo hapa na wazazi wao hawapo, hivyo tunajaribu kutafuta wazazi wa watoto hawa. Na watu wote hawa mnaowaona wanajaribu kupata msaada wa kuwasaidia.” 

Wadau wa misaada ya kibinadamu wanajaribu kwa kila hali kukusanya rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na mahitaji ya dharura yanayohitajika haraka kama vile malazi, maji, huduma za usaji na kujisafi, ulinzi, huduma za afya, chakula na lishe.