Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi waliosalia nchini Ukraine waendelea kufikishiwa misaada na Umoja wa Mataifa

Wakaazi wa eneo la Luhanska mashariki mwa Ukraine wanapokea msaada kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo. (Maktaba)
FAO Ukraine
Wakaazi wa eneo la Luhanska mashariki mwa Ukraine wanapokea msaada kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo. (Maktaba)

Wananchi waliosalia nchini Ukraine waendelea kufikishiwa misaada na Umoja wa Mataifa

Msaada wa Kibinadamu

Uvamizi wa Urusi  nchini Ukraine umefurusha makwao mamilioni ya watu kwenda kusaka hifadhi maeneo ya mikoani na hata nchi jirani. Katika Mkoa wa Donetsk asilimia 90 ya wananchi walikimbia tu vita ilipoanza, na zaidi ya wananchi 1,000 walioamua kusalia hawana huduma za maji, umeme na gesi na Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kila juhudi kuhakikisha wanapata huduma hizo muhimu. 

Wakazi wa Chasiv Yar mkoani Donetsk tangu kuibuka kwa vita kati ya Ukraine na Urusi wamekuwa wakiishi katika hali ya taabu na kujificha katika mahandaki chini ya nyumba zao.

Mapigano yameharibu nyumba zao pamoja na miundombinu na kuwaacha wakazi zaidi ya 1,000 wakiwa katika hali ngumu.

Mfanyakazi wa kujitolea aitwaye Oleksandr anasema baadhi ya walioamua kubaki katika eneo hilo wanawasaidia wananchi wenzao kwani kuna kundi kubwa la wazee wake kwa waume ambao hawataki kuondoka na wanahitaji msaada, 

“Kwa wakati huu, tuseme, hali si rahisi. Naweza kusema kuwa ni ngumu kwa wenyeji. Kwa nini? Hakuna umeme, gesi, taa, wala miundombinu ya kuletajoto kwenye nyumba. Ndio maana shirika letu linafanya kila liwezalo kusaidia watu kuboresha nyumba zao.”

Mratibu mkazi wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Denise Brown amefika katika mkoa huo akiwa na msafara wa 31 uliosheheni misaada ya kibinadamu kutoka kwa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na kugawa misaada hiyo kwa wananchi.

Miongoni mwa waliopokea msaada ni Bi. Lyubove, “Tumepokea misaada ya kibinadamu leo, sijui imetoka wapi, lakini kila mtu amepata chupa tatu za maji pamoja na masanduku mawili ya bidhaa.”

Pamoja na kushukuru kwa msaada huo Bi.Lyubove akatoa ombi kwa wadau wa misaada ya kibinadamu, “Kodi ya nyumba ni ghali sana kwa sasa. Watu wameanza kurejea Chasiv Yar. Ingawa ni ngumu sana na inatisha kuishi hapa lakini wanajaribu kurudi nyumbani hasa wale wenye nyumba zao binafsi zilizo ambazo zina majiko. Majira ya baridi yanakuja, na watu hawana pesa za kulipa… Pensheni ni ndogo, na hakuna mishahara.”

Kiujumla kwa mwaka huu Umoja wa Mataifa na wadau wake wamefanikiwa kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wakazi zaidi ya milioni 8.3 nchini Ukraine.