Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwezekano wa DRC na Rwanda kuzozana moja kwa moja ni dhahiri

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu Huang Xia akizungumza katika Baraza la Usalama
UN Photo/Eskinder Debebe
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu Huang Xia akizungumza katika Baraza la Usalama

Uwezekano wa DRC na Rwanda kuzozana moja kwa moja ni dhahiri

Amani na Usalama

Hivi sasa dalili za mzozano wa moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Rwanda zi wazi  kutokana na pande hizo kuendelea kulaumiana juu ya uungaji mkono wa makundi yaliyojihami Mashariki mwa DRC, wakati huu ambapo hali ya amani inazidi kuzorota. 

Ni kauli ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu wa Afrika, Huang Xia aliyotoa leo akiwasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa Makubaliano yam waka 2013 kuhusu Amani, Usalama na Ushirikiano kwa ajili ya DRC na Ukanda huo ikigusia kipindi cha kuanzia tarehe 16 Machi hadi 15 Septemba mwaka huu wa 2023. 

Bwana Huang amesema miezi 6 tangu awasilishe ripoti Barazani, hali ya kibinadamu haijaimarika. Kwa upande mwingine: katika sehemu ya Mashariki ya DRC tunashuhudia kuanza tena kwa uhasama mkubwa kwenye miji ya Masisi na Rutshuru, jimboni Kivu Kaskazini. 

Mjumbe huyo anasema upande mmoja unalaumiwa kuunga mkono wapiganaji wa M23 ilhali upande mwingine unalaumiwa kuunga mkono jeshi la Kidemokrasia kwa Ukombozi wa Rwanda (FDLR). 

Hofu zaidi ya pande mbili hizo kuzozana zaidi ni kwa kuzingatia kwamba kila upande, yaani Rwanda na DRC unajiimarisha kijeshi na hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati yao huku kauli za chuki zikizidi kila uchao. “Hizi ni dalili za kutia hofu kubwa na hatuwezi kuzipuuza.” 

Idadi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC nayo imeendleea kuongezeka na kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR hii leo Oktoba 17, zaidi ya watu 90,000 katika maeneo ya Rutshuru na Masisi wamelazimika kukimbia makazi yao katika wiki za kwanza za Oktoba.  

Rwanda: Tatizo Mashariki ya DRC ni kutong’oa “mzizi wa chuki” 

Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Claver Gatete, amesema hali ya sasa imesababishwa na kushindwa kushughulikia mzizi wa matatizo Mashariki mwa DRC akisema hicho ndio kichocheo cha kuendelea kwa mzozo. 

Amesema kwa miongo mitatu iliyopita, eneo la Mashariki mwa DRC limesalia kuwa mazalia ya vikundi vilivyojihami ambavyo vinaleta vurugu sio tu DRC bali pia nchi jirani. 

DRC: M23 iliondoka chumba cha mkutano Nairobi 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, haikunyamaza kwani Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Zénon Mukongo Ngay, amesema mwelekeo wa mazungumzo na Rwanda uko wazi. 

Amesema mwelekeo huo unaelezea hatua za kufikia mazungumzo. “Na sisi tunafahamu hilo wazi – upokonyaji silaha kikundi cha M23 na uvunjaji wa kikundi hicho, kurejea kwa wakimbizi wa ndani ambao hapa tumejadili kiwango cha janga lililoko. Hiyo ndio njia ya mwelekeo wa kuwa na mazungumzo na Rwanda.” 

Balozi Ngay amesema kwa mpango wa Mchakato wa Nairobi, unaoratibiwa na Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, EAC, yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wa mchakato huo. 

“Mimi nilikuwa mmoja wa wajumbe wa mchakato huo Mh. Rais. M23 ilikuwa mjumbe wa mashauriano hayo mjini Nairobi. Waliondoka chumba cha mkutano n kuenda kuanza mapigano wakati tunajadili na vikundi vingine vilivyojihami,” amesema Balozi Ngay.