UN na Tanzania kuendeleza ushirikiano – Balozi Huang 

6 Mei 2021

Umoja wa Mataifa umeipongeza Tanzania kwa mchango wake katika juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali ya mapigano duniani. 

Kauli hiyo imetolewa na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jijini Nairobi nchini Kenya. 

Mazungumzo kati ya Rais Samia na Balozi Huang yamefanyika jijini Nairobi wakati kiongozi huyo wa Tanzania alipokuwa ziarani kwa siku mbili. 

Bwana Huang amesema “Umoja wa Mataifa unaahidi kuwa utaendelea kushirikiana na Tanzania kulinda amani ili maendeleo ya jamii na uchumi yastawi.” 

Kwa upande wake Rais Samia amesema “hali ya ulinzi na usalama nchini Tanzania ni nzuri na ameomba Umoja wa Mataifa kuendeleza jitihada za kulinda amani na usalama katika maeneo yote yenye mizozo.” 

Halikadhalika ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kushawishi Muungano wa Ulaya kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Burundi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter