Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaanza kugawa misaada ya chakula kwa wahitaji Gaza

Mfanyikazi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) akigawa mkate kwa familia iliyohifadhiwa katika shule ya Umoja wa Mataifa huko Gaza.
© WFP/Ali Jadallah
Mfanyikazi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) akigawa mkate kwa familia iliyohifadhiwa katika shule ya Umoja wa Mataifa huko Gaza.

WFP yaanza kugawa misaada ya chakula kwa wahitaji Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Ikiwa leo ni siku ya tano ya mzozo kati ya Israeli na Palestina huko Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamepiga kambi kuhakikisha yanafikisha misaada kwa wahitaji wakati huu ambapo mapigano hayo yamefurusha takribani watu 246, 000 kutoka ukanda wa Gaza pekee.

Mashirika hayo ni pamoja na lile la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP ambalo limeanza kugawa mikate, vyakula vya makopo na vingine vilivyo tayari kuliwa kwa takribani watu 100,000 waliosaka hifadhi kwenye maeneo ya hifadhi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA huko Gaza. 

Lengo la UNRWA ni kwamba operesheni hii ya dharura ifikishe misaada kwa zaidi ya watu 800,000. Ikumbukwe kuwa idadi hii ni pamoja na wakimbizi wa zamani waliokuwa wanahifadhiwa na UNRWA.

Mkurugenzi Mkazi wa WFP  huko Palestina Samer Abdeljaber anasema tuko hapa kwenye enep na tunafanya  kila tuwezalo kuhakikisha wahitaji waliofurushwa makwao ambao wanaishi kwenye makazi ya muda wanapata chakula na msaada wanaohitaji ili waweze kuishi. Tutaanza pia kutoka vocha za fedha ili watu waweze kununua chakula kutoka kwenye maduka yaliyo bado wazi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nalo pia liko Gaza likisambaza misaada ya kiutu.

WFP inasihi pande kinzani kuhakikisha njia za usambazaji chakula ziko wazi ili misaada ifikie wahitaji huku ikitoa ombi la dola milioni 17.3 ili kufanikisha operesheni zake za dharura kwa wiki nne zijazo kwani mzozo huu umelipuka wakati tayari ukata ulikuwa unalikabili na kulazimu mwezi Juni kukata misaada kwa maelfu ya familia za kipalestina zisizo na uwezo.

Wakati huo huo UNRWA kupitia mtandao wa X inasema tangu Jumamosi hadi hii leo watumishi wake 9 wameuawa kwenye mashambulizi hayo huko Gaza.