Gaza: Siku ya nne bila mapigano misaada muhimu yafika kaskazini
Gaza: Siku ya nne bila mapigano misaada muhimu yafika kaskazini
Raia wa Gaza waliokata tamaa kaskazini mwa eneo hilo, leo Jumatatu Nov 27 wamepata maji safi kwa mara ya kwanza katika muda wa wiki kadhaa huku kusitishwa kwa mapigano kukiwezesha kupanua upatikanaji wa misaada katika Ukanda huo, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA.
Na kama OCHA, ilivyoripoti kwamba watu wa kusini walikuwa wakipanga foleni kwa kilomita nyingi kupata gesi ya kupikia na kukimbilia kuchoma fremu za madirisha na milango kwa ajili ya kupikia, imeongeza kuwa kusitisha kwa siku nne mapigano kama ilivyokubaliwa na Israel na Hamas "imedumishwa kwa kiasi kikubwa".
Chini ya makubaliano hayo, Hamas iliwaachilia mateka 17 zaidi waliotekwa nyara wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo lililokuwa na silaha kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na kufanya idadi ya mateka walioachiwa huru kufikia 58, OCHA imesema. Wapalestina wapatao 117 wanaoshikiliwa katika jela za Israel pia wameachiliwa huru tangu Ijumaa.
Wakati huo huo mwishoni mwa wiki juhudi mpya za kuimarisha mfumo wa huduma ya afya ulioharibiwa wa Gaza zilitimia wakati msafara wa Umoja wa Mataifa ulisafirisha chanjo za kuokoa maisha kutoka Gaza (Gaza City) hadi kusini mwa eneo hilo, ambapo zinaweza kuhifadhiwa kwenye jokofu.
OCHA jana Jumapili imesema msafara wa pamoja wa Umoja wa Mataifa ulikusanya dozi 7,600 za chanjo za magonjwa mbalimbali kutoka ghala la Wizara ya Afya ya Gaza, ambapo zingekuwa hazitumiki kwa sababu ya ukosefu wa friji kaskazini, na kufanikiwa kuzileta kusini.
"Baada ya ukaguzi wa kina ili kuhakikisha kama bado ziko sawa, chanjo zitatumika kuimarisha uchanjaji wa kawaida, ambao umetatizwa na uhaba wa vifaa na uhasama unaoendelea," OCHA imesisitiza.
"Njaa, kukata tamaa na uharibifu"
Wasaidizi wa kibinadamu waliofika kaskazini mwa Ukanda huo kwa mara ya kwanza tangu ulipofungwa na operesheni za kijeshi za Israel wiki zilizopita wameshuhudia matukio ya ukiwa. Jumapili, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wamefanya kazi ya pamoja ya kupeleka msaada muhimu wa chakula katika hospitali ya Al-Ahli katika mji wa Gaza na maeneo jirani.
"Ni hatua ya matumaini, lakini timu ilikutana na simulizi za uchungu kutoka kwa watu ambao hawajapokea msaada wowote kwa wiki kadhaa," Mwakilishi wa WFP katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu Samer AbdelJaber, ameandika kwenye jukwaa la kijamii X. "Waliona njaa, kukata tamaa na uharibifu. .”
Jumamosi shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) na ujumbe unaoongozwa na Chama cha Hilali Nyekundu cha Palestina (PRCS) waliwahamisha takriban wagonjwa 17 na majeruhi kutoka hospitali ya Al-Ahli pamoja na wenzao 11, hadi katika hospitali inayofahamika kama European Hospital huko Khan Younis kusini mwa Gaza. Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa wagonjwa walikuwa "wanakabiliwa na majeraha ya risasi, kukatwa viungo na kuchomwa moto". Kiongozi huyo anarejerea wito wa "kuendea kusitishwa kwa mapigano".
Msaada wa haraka wa chakula
Jumapili, misafara ya misaada ilileta chakula kilicho tayari kuliwa kwenye makazi manne yanayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza, pamoja na mahema, blanketi na maji ya chupa.
"Misafara hiyo ilikaguliwa kwa uangalifu na vikosi vya Israeli vilivyowekwa katika kituo cha ukaguzi karibu na Wadi Gaza kabla ya kuelekea kaskazini," OCHA imesema.
Tangu tarehe 24 Novemba, WFP imeweza kutoa msaada muhimu wa chakula kwa watu 110,000 katika makazi ya UNRWA na jumuiya zinazowapokea kupitia usambazaji wa mkate, vifurushi vya chakula, na vocha za kielektroniki.