Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP Imeanza tena usambazaji wa msaada wa chakula Ethiopia

Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.
WFP Ethiopia
Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.

WFP Imeanza tena usambazaji wa msaada wa chakula Ethiopia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limeanza kusambaza chakula kwa wakimbizi takriban 900,000 nchini Ethiopia, na kwa kuwapa msaada wa kibinadamu wakimbizi kutoka nchini Sudan. 

Familia zinazoishi katika kambi za wakimbizi katika mikoa 5 ikiwa ni pamoja na wakimbizi wapya wanaowasili ambao wamekimbia nchi yao wanapokea vifurushi vya chakula kwa mara ya kwanza tangu WFP kusitisha ugawaji wa chakula mwezi Juni mwaka 2023, kufuatia ripoti za uporaji wa msaada wao kwa kiasi kikubwa.

Valerie Guarnieri, mkurugenzi mtendaji msaidizi wa WFP amesema  “Wafanyakazi wa WFP na wadau wetu wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha ili kuhakikisha kwamba tunaweza kutoa chakula kwa wale wanaokihitaji zaidi. Chakula ni tegemeo kwa wakimbizi wanaoishi katika hali ngumu sana, na tumaini ni kwamba sasa tuna hatua za kurejesha msaada muhimu,”. 

Chakula kimesambazwa kwa watu wa mkoa wa Afar nchini Ethiopia
© WFP/Claire Nevill
Chakula kimesambazwa kwa watu wa mkoa wa Afar nchini Ethiopia

Idadi ya waliokimbia Sudan na kuingia Ethiopia

WFP imesema takriban watu 35,000 ambao wamekimbia kutoka Sudan na kuingia Ethiopia katika kipindi cha miezi 6 iliyopita wanahitaji msaada wa haraka wa chakula. 

Hali kadhalika Ethiopia pia inawahifadhi wakimbizi wengine 850,000 wengi wao kutoka Somalia, Sudan Kusini na Eritrea. 

Usambazaji wa chakula unaoongozwa na WFP utaanza tena katika mikoa ya Somalia, Gambella, Benishangul Gumuz, Oromia, SNNP na Afar, msaada ambao unajumuisha ugawaji wa nafaka, kunde, mafuta ya mboga na chumvi. Wakimbizi wengine shirika hilo limesema watapokea msaada wa pesa taslimu. 

Kurejeshwa kwa usambazaji wa chakula kwa wakimbizi kunafuatia mageuzi makubwa katika kambi zote nchini humo.

Msafara wa malori ya WFP yakipeleka chakula na lishe kwa Adi Harush, Mai Aini, Mekelle na Shire huko Tigray, Ethiopia.
WFP Ethiopia
Msafara wa malori ya WFP yakipeleka chakula na lishe kwa Adi Harush, Mai Aini, Mekelle na Shire huko Tigray, Ethiopia.

Mageuzi hayo ni pampja na 

 ·   Maghala yote 24 katika kambi za wakimbizi sasa yanasimamiwa na WFP pekee

·   Wakimbizi sasa watasajiliwa kidijitali ili kupata msaada kupitia dhana ya ufuatiliaji wa usambazaji  ulimwenguni ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

·   Mifumo iliyoimarishwa ya maoni na kuripoti kwa wakimbizi, ikijumuisha madawati ya msaada kwenye tovuti na kupitia nambari ya simu isiyojulikana.

·    Mashirika ya ziada yasiyo ya kiserikali yameajiriwa na kupatiwa mafunzo na WFP ili kuimarisha usambazaji wa chakula.

·    Taratibu mpya na za kina za ukusanyaji wa chakula zitahakikisha kwamba wakimbizi wanapokea stahiki zinazofaa kila wakati. 

Vile vile, WFP imechukua hatua zinazohitajika ili kuanza tena usambazaji wa chakula kwa mamilioni ya Waethiopia wasio na chakula. 

Watoto wadogo wasichana wakila chakula kilichoandaliwa na programu ya shirika la chakula la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya chakula shuleni (Maktaba)
WFP/Michael Tewelde
Watoto wadogo wasichana wakila chakula kilichoandaliwa na programu ya shirika la chakula la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya chakula shuleni (Maktaba)

Kushirikiana na wadau wengine

Hatua hizo ni pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano na jamii ili kutambua na kulenga watu walio hatarini zaidi na kuwasajili kidijitali ili wapate usaidizi haraka. 

Pia inajumuisha utaratibu ulioimarishwa wa vifaa na usambazaji unaoruhusu ufuatiliaji sahihi zaidi hadi kwa kila familia inayofadhiliwa.  

Pia WFP imesisitiza kuwa kurejesha usambazaji wa msaada wa chakula kwa wakimbizi ni muhimu. 

Takwimu za hivi karibuni za hali ya njaa nchini humo zinaonyesha kuwa uhakika wa chakula kwa wakimbizi umezorota katika miezi iliyopita, na kusababisha kuongezeka kwa utapiamlo, mvutano mkubwa katika kambi za wakimbizi na hata safari zisizo salama za kurejea mpakani.