Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chad imewakirimu wakimbizi kwa kila kitu, sasa imeishiwa inahitaji msaada pia: WFP

Umati mkubwa wa wakimbizi, wakiwemo wanaume, wanawake, na watoto, wanakusanyika kuzunguka malori ya WFP kwa ajili ya usambazaji wa chakula katika eneo kame.
© WFP/Jacques David Wakimbizi wa Sudan wakipokea msaada wa chakula kutoka wa WFP nchini Chad

Chad imewakirimu wakimbizi kwa kila kitu, sasa imeishiwa inahitaji msaada pia: WFP

Amani na Usalama

Chad ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya milioni ambao sasa umekuwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na unaokuwa kwa kasi barani Afrika kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP. 

Shirika hilo linasema na vita inayoendelea katika nchi jirani ya Sudan imeongeza shinikizo la rasilimali na mahitaji ya kibinadamu kwani maelfu kwa maelfu ya watu zaidi wanavuka mpaka na kusaka usalama Chad. 

Katika kituo cha wakimbizi  cha Adre mpakani  mwa Chad hekaheka ni nyingi kwani wakimbizi wanamiminika kwa idadi kubwa wakiwa na virago vyao wanakimbia vita inayoendelea Sudan, na miongoni mwao ni Roukaya Yacoub mama wa watoto saba aliyelazimika kukusanya kile alichoweza na wanawe na kuchanja mbuga baada ya mumewe kuawa katika shambulio lilitokea Ardamata.

Sasa yuko kambini hapa lakini jinamizi la shambulio hilo linaendelea kumuandama “Walitushambulia kwa siku tatu mfululizo, ilikuwa mbaya sana, walikwenda mlango kwa mlango wakiwakusanya wanaume wakiwatoa nje na kuwaua. Walimwita baba watoto wangu atoke nje na kisha wakampiga risasi na kumuua. Walichukua kila kitu tulichokuwa nacho na sasa nimesalia mkavu sina chochote cha kuwasaidia wanangu. Hatukuwa na chaguo linguine bali kukimbilia Chad.”

Mfanyakazi wa UNHCR aliyevaa fulana ya bluu akimshika mkono mvulana mdogo wanapotembea na wakimbizi wengine kuelekea lori kubwa katika eneo la kuhamishiwa nchini Chad.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune Wakimbizi kutoka Sudan wanahamishwa kutoka kambi kwa kambi nchini Chad.

Kwa mujibu wa WFP ongezeko hili la wakimbizi limezidisha shinikizo la mahitaji ya kibinadamu kama chakula inachokigawa ambacho ndio tegemeo pekee la wakimbizi hawa na sasa hakitoshelezi tena kwani idadi ya watu inaongezeka kila uchao, rasilimali zinakwisha na kuyaacha mashirika ya misaada ya kibinadamu yakihaha na kukosa la kufanya.

Changamoto za wakimbizi hawa pia zinajumuisha masuala ya kiafya ikiwemo utapiamlo kwa watoto, majeruhi na magonjwa mengine ambayo baada ya vipimo wanahitaji msaada. Pierre Honnorat ni mkurugenzi wa WFP nchini Chad anasema “Wachad wamegawana na wakimbizi kila walichokuwa nacho sasa hawana tena cha kugawana. Wao wenyewe wanahitaji msaada, hivyo tunahitaji kuwasaidia wakimbizi wote 600,000 waliokuja, wakimbizi wa Chad wanaorejea lakini pia sasa tunahitaji kuwasaidia Wachad wanaohifadhi wakimbizi ambao nao wanahaha kama walivyo waliowasili toka Sudan.”

WFP inasema zaidi ya watu nusu milioni wamevuka mpaka tangu Aprili wakiwemo wakimbizi 45,000 na watu 80,000 raia wa Chad wanaorejea na idadi ya wanaoingia Chad inatarajiwa kufikia watu 600,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu