Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: UNICEF na Save the Children wataka shule zifunguliwe katika maeneo yenye usalama

Watoto wa Sudan waliopoteza makazi yao wakiwa kwenye makazi ya muda.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Watoto wa Sudan waliopoteza makazi yao wakiwa kwenye makazi ya muda.

Sudan: UNICEF na Save the Children wataka shule zifunguliwe katika maeneo yenye usalama

Amani na Usalama

Ikiwa ni takriban miezi sita sasa tangu kuibuka kwa mzozo nchini Sudan, inakadiriwa watoto milion 19 sawa na mtoto 1 kati ya 3 hawapo shuleni kutokana na vita. 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusina na masuala ya watoto UNICEF pamoja na Shirika la Save the children wametoa taarifa hiyo ya pamoja hii leo huko Port Sudan ambapo wamebainisha kuwa takriban watoto milioni 6.5 wamepoteza fursa ya kwenda shuleni kutokana na ukosefu wa usalama na angalau shule 10,400 zimefungwa katika maeneo yaliyoathirika na mzozo. 

UNICEF na Save the Children pia wametoa wito kwa mamlaka za Sudan kufungua upya shule katika maeneo salama, huku zikiunga mkono mbinu mbadala za kujifunza katika jamii ambazo shule haziwezi kufunguliwa tena kwa sababu ya usalama na usalama.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Mandeep O’Brien amesema Sudan ipo ukingoni kukumbwa na mzozo mbaya zaidi wa elimu duniani. “Ni nusu mwaka sasa watoto wanakabiliwa na vitisho vya vita. Sasa wamelazimishwa kuwa nje ya madarasa yao, walimu wao, marafiki zao, wapo katika hatari ya kudumbukia kwenye dimbwi linalohatarisha mustakabali wa maisha yao ya baadae.”

Zaidi ya watoto milioni 5.5 ambao wanaishi katika maeneo ambayo hayakuathiriwa sana na vita wanasubiri mamlaka za mitaa kuthibitisha kama madarasa yanaweza kufunguliwa tena.

Hata kabla ya vita kuanza mwezi April 2023 nchini Sudan, takriban watoto milioni 7 walikuwa nje ya shule wakikabiliwa na umasikini na ukosefu wa utulivu. 

Iwapo vita itaendelea nchini humo hakuna mtoto wakisudan anatakaye weza kurejea shuleni na hali hii itawaletea madhara kwa maisha yao katika kipindi cha muda mfupi na maisha ya baadae na kuwaweka hatarini kwenye masuala hatari ikiwemo kuandikishwa kwenye makundi ya wapiganaji na unyanyasaji wa kijinsia. 

Naye Mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Sudan Arif Noor amesema tangu mzozo huo uanze, Sudan imeibuka kama mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani duniani, huku ukiwa na wakimbizi wa ndani milioni 4.4, idadi hiyo ikiwa ni pamoja na karibu watoto milioni 2.5. 

“Zaidi ya hayo, watoto milioni 5 wenye umri wa kwenda shule wanajikuta wamenaswa katika maeneo yenye migogoro, na kuwaweka katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza fursa muhimu ya elimu na huduma muhimu za ulinzi," alisema Noor.

Mbali na kujua kusoma kuandika na kuhesabu, watoto wakiwa shuleni hujifunza stadi za kijamii na kihisia ambazo katika wakati wa migogoro zinaweza kuwa tegemeo la kukabiliana na vurugu na kiwewe. Wakati huo huo, wanaweza pia kufikia huduma nyingine nyingi muhimu za kuokoa maisha kama vile lishe, huduma za afya, na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.

UNICEF na Save the Children wanafanya kazi kwakushirikiana na wadau wengine kuhakikisha mamilioni ya watoto wa Sudan wanaweza kupata elimu bora na kurejea shuleni kwa usalama hivi karibuni kabla ya mwaka wao wa masomo kuathiriwa.