Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yalaani mashambulizi katika shule huko Gaza 

Walinda amani UN waliovaa kofia za bluu wakizungumza na wafanyakazi wa matibabu katika Hospitali ya Shifa huko Gaza.
WHO Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini misaada ya kibinadamu, ikiongozwa na WHO ilifika katika Hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza ili kutathmini hali ilivyo.

Mashirika ya UN yalaani mashambulizi katika shule huko Gaza 

Amani na Usalama

Kufuatia makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi dhidi ya shule mbili huko Gaza hii leo, mashirika ya Umoja wa Mataifa wamesisitiza haja ya kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya shule na kutolenga watoto, makazi ya watu, na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu.

Tweet URL

Adele Khodr ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kupitia mtandao wa kijamii wa X kuwa matukio ya mauaji na uharibifu kufuatia mashambulizi dhidi ya shule za Al-Fakhoura na Tal Al-Zaatar huko Gaza - ambayo yalisababisha vifo vya watoto na wanawake wengi - ni vya kutisha na kuhuzunisha.

Bi Khodr amesisitiza haja ya kukomesha mashambulizi haya ya kutisha mara moja na kwamba watoto, shule na makazi sio walengwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema kupitia mtandao wake wa X kuwa “Tunaona picha za kutisha za watoto na raia wakiuawa huko #Gaza - kwa mara nyingine tena - wakati wakipata hifadhi katika shule ambayo inapaswa kulindwa kila wakati," 

Alisisitiza hitaji la kukomesha mauaji, uharibifu na mateso, na kukomesha kile alichokiita "ndoto hii mbaya ambayo watoto wanapitia sasa."

Akizungumzia mashambulizi hayo, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini amesema kwamba amepokea “picha na video za kutisha za makumi ya watu waliofariki na kujeruhiwa katika shule nyingine ya UNRWA ambapo maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wanahifadhi katika shule hiyo huko Ukanda wa kaskazini wa Gaza.”

Naye pia amesisistiza haja ya mashambulizi haya yasiwe jambo la kawaida, akiwataka kuacha na kueleza usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu hauwezi kusubiri tena.

Mashambulizi kwenye shule

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, msemaji wa UNRWA Adnan Abu Hasna, amesema kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, karibu watu 200 waliuawa na kujeruhiwa katika shule ya Al-Fakhoura hii leo.

“Hatujui takwimu kamili na ikiwa idadi itaongezeka au la,” alisema, na kuongeza kuwa mashambulizi hayo yametokea katika shule ya UNRWA na pande zote kwenye mzozo zinajua kuwa eneo hilo linawahifadhi mamia ya Wapalestina.

Akielezea kuhusu kuongezeka kwa mahitaji amesema anaona mamia ya watoto wakiomba chakula na maji na maelfu ya watu wakiwa kwenye foleni za maji masafi. 

“Mambo yanazidi kuwa mabaya,”" alisema. “Tunazungumzia janga huko Gaza.”

Mtengenezaji wa filamu Bisan Ouda, hospitali ya Al-Shifa, Gaza, idara ya watoto wachanga, mama wa Palestina, watoto, mtoto mchanga, huduma ya afya, mgogoro wa kibinadamu
© Bisan Ouda for UNFPA Familia zinapata makazi katika hospitali ya Al shifa ( Maktaba)

Hospitali ya Al-Shifa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO limetuma ujumbe wake kutembelea hospital ya Al -Shifa ambayo imezingirwa na wapiganaji ambapo maelfu ya raia walikuwa wakijihifadhi hapo pamoja na wahudumu wa afya ambao walikuwa wakihangaika kuhudumia wagonjwa.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ujumbe huo uliwasiliana na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) ili kuhakikisha wanapita kwa usalama katika njia waliyokubaliwa, hata hivyo, akaeleza hii ilikuwa “operesheni hatari” katika eneo lenye migogoro, na mapigano makali yakiendelea maeneo ya karibu na hospitali.

“Timu iliona hospitali haiwezi kufanya kazi tena: hakuna maji, hakuna chakula, hakuna umeme, hakuna mafuta, vifaa vya matibabu vikiwa vimepungua,” alisema Dkt. Tedros na kuongeza kuwa “Kutokana na hali hii ya kusikitisha na hali ya wagonjwa wengi, wakiwemo watoto wachanga, wahudumu wa afya waliomba msaada wa kuwahamisha wagonjwa ambao hawawezi kupata huduma ya kuokoa maisha huko tena.”

WHO imesema kuna wahudumu wa afya 25 na wagonjwa 291 waliosalia katika hospital ya Al-Shifa, na vifo vya wagonjwa kadhaa vimetokea katika siku mbili hadi tatu zilizopita kutokana na kuzimwa kwa huduma za matibabu. 

Wagonjwa hao ni pamoja na watoto 32 walio katika hali mbaya sana, watu wawili walio katika uangalizi maalum bila kuwa na huduma ya mashine za kusaidia kupumua na wagonjwa 22 wa kusafisha figo - dialysis ambao upatikanaji wao wa matibabu ya kuokoa maisha umetatizwa pakubwa. Idadi kubwa ya wagonjwa ni waathirika wa kiwewe cha vita.

WHO na wadau wake wanaandaa mipango ya haraka kwa ajili ya kuwahamisha wagonjwa waliosalia, wafanyakazi na familia zao. Katika muda wa saa 24 hadi 72 zijazo, ikisubiriwa hakikisho la kupitishwa kwa usalama kwa wahusika kwenye mzozohuo, misheni ya ziada inapangwa kusafirisha wagonjwa kwa haraka hadi hospital iliyopo kusini mwa Gaza.

“Tunaendelea kutoa wito wa ulinzi wa afya na raia,” alihimiza Mkuu wa WHO. “ Hali ya sasa haiwezi kuvumilika na haikubaliki.”