Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SDGs zilikuwa 'mdomoni' mwa kila mtoa hotuba – Rais UNGA78

Rais wa Baraza Kuu la UN Balozi Dennis Francis akiwapatia waandishi wa habari tathmini ya vikao vya ngazi ya juu vya mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN (UNGA78).
UN /Eskinder Debebe
Rais wa Baraza Kuu la UN Balozi Dennis Francis akiwapatia waandishi wa habari tathmini ya vikao vya ngazi ya juu vya mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN (UNGA78).

SDGs zilikuwa 'mdomoni' mwa kila mtoa hotuba – Rais UNGA78

Masuala ya UM

Kile nilichoshuhudia ni jamii ya kimataifa iliyojizatiti upya kukamilisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ifikapo mwaka 2030, amesema Rais wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78, Dennis Francis akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo.

Kilichomtia matumaini Balozi Francis

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani baada ya kumalizika kwa vikao vya ngazi ya juu vya UNGA78, Balozi Francis amesema alitiwa moyo na hotuba za wakuu wa nchi na serikali pamoja na wawakilishi wa jumla ya nchi 189 wanachama wa Umoja wa Mataifa waliopanda kwenye mimbari ya ukumbi adhimu wa Baraza Kuu na kuhutubia.

Katika kila midomo ya mtoa hotuba, Ajenda ya 2030 ilitajwa kwa sababu ya umuhimu wa maendeleo endelevu kwa ustaarabu na sayari, amesema Rais huyo wa UNGA78.

Kilichomtia furaha zaidi ni kuwa kuweko kwa utashi na nia njema ya kuona Umoja wa Mataifa inatekeleza SDGs.

Wapiganaji Karabakh zingatieni sheria

Alipoulizwa hali inayoendelea kwenye eneo la Karabakh linalogombaniwa na Armenia na Azerbaijan, Balozi Francis amesihi wapiganaji kokote kule waliko wazingatie sheria ya kimataifa kwa sababu ya athari za janga la kibinadamu na machungu wapatayo wale ambao makombora yanawaangukia, sio tu wapiganaji bali pia raia.

Mchakato wa kurekebisha Baraza la Usalama

Balozi Francis akaulizwa pia marekebisho ya Baraza la Usalama ambapo amesema “tunahitaji kufikiria upya muundo wa Baraza la Usalama ili liweze kuendana na uhalisia na siasa za sasa za dunia. Huo utakuwa ni mchakato ambao utaendelea ndani ya Baraza kwa muda.”

Hata hivyo amesema vyovyote vile itakavyokuwa matokeo, Chata ya Umoja wa Mataifa inaeleza bayana jukumu la Baraza la Usalama, na kile ambacho tunahitaji ni Baraza la Usalama linalokidhi mahitaji na lililo tayari na lenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake, bila kujali mchakato utachukua muda gani.

Wanawake na wasichana Afghanistani

Waandishi wa Habari walitaka kufahamu msimamo wake kuhusu Afghanistani ambako hali ya ustawi wa wanawake iko mashakani chini ya watalibani ambapo amesema “wanawake na wasichana wana haki zisizopokonyika, haki za binadamu ambazo zinapaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa.”

Amesihi watalibani kufikia upya será na kuruhusu wasichana waende shule, wapate elimu ili nao waweze kutekeleza wajibu wao wa maendeleo kwenye jamii zao. “wanaweza kuongeza thamani na kuifanya Afghanistani kuwa taifa thabiti na lenye utengamano.”