Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yatangaza mlipuko mpya wa kipundupindu, WHO yachukua hatua kusaidia

WHO inawasaidia wahudumu wa afya wa Sudan kwa kuwapatia madawa muhimu, msaada wa manusura na vifaa vya upasuaji, na mafuta ili kudumisha huduma za afya.
© WHO/Lindsay Mackenzie
WHO inawasaidia wahudumu wa afya wa Sudan kwa kuwapatia madawa muhimu, msaada wa manusura na vifaa vya upasuaji, na mafuta ili kudumisha huduma za afya.

Sudan yatangaza mlipuko mpya wa kipundupindu, WHO yachukua hatua kusaidia

Afya

Sudan imetangaza mlipuko mpya wa kipindupindu katika jimbo la Gedaref ambako kuna wagonjwa 264 wanaohisiwa kuwa na kipundupindu, wanne wamethibitishwa na vifo 16 vinavyohusishwa na ugonjwa huo vimeripotiwa kwa mujibu wa taarifa ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo.

Shirika hilo limesema hivi sasa uchunguzi unaendelea ili kubaini endapo kipindupindu kimesambaa pia katika majimbo mengine ya Khartoum na Kordofan Kusini ambako wagonjwa wengi wa ugonjwa wa kuhara kutokana na maji wameripotiwa.

Dkt. Nima Abid, mwakilishi wa WHO nchini Sudan, ametembelea jimbo la Gedaref tarehe 17 Septemba 2023 na kukutana na mamlaka za afya na washirika ili kuratibu hatua za kuchukua. 

Amessema "Fursa ya ufikiaji watu bila vikwazo katika maeneo yaliyoathiriwa na maeneo jirani ni muhimu ili kukabiliana vyema na mlipuko huu unaoendelea. Mlipuko wa kipindupindu unaweza kuwa na athari mbaya katika muktadha wa mfumo wa afya ambao tayari umelemewa kwa sababu ya vita, uhaba wa vifaa vya matibabu na wafanyikazi wa afya, utapiamlo na changamoto za ufikiaji."

WHO inaisaidia Sudan hata kabla ya mlipuko

Hata kabla ya mlipuko huo kutangazwa, WHO ilikuwa tayari imetoa vifaa vya kipindupindu, ikiwa ni pamoja na dawa za kuua vijiuavijasumu, dawa ya kuongeza maji mwilini na drip kwa majimbo 6, yakiwemo Gedaref, Khartoum na Kordofan Kusini, pamoja na vifaa vya kupima na uchunguzi wa haraka kwa majimbo yote 18 ya Sudan. WHO pia ilikuwa ikisaidia vituo 3 vya kuwatengwa na kipindupindu katika Jimbo la Gedaref na viwili 2 kati ya hivyo kwa dawa na vifaa vya afya, na kusaidia kikamilifu kituo cha mwisho kwa utoaji wa vifaa vya huduma na vifaa vya matibabu.

Mapema mwaka huu, zaidi ya wafanyakazi 2800 wa afya wa Sudan walishiriki katika mafunzo ya mtandaoni ya kuwajengea uwezo yaliyoendeshwa na WHO kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa kuhara wakati wa shida ya maji. 

Kozi nyingine ya mtandaoni kuhusu kipindupindu, homa ya kidingapopo na itifaki ya kudhibiti malaria, ilifanyika wiki hii, kwa zaidi ya wafanyakazi 8000 wa afya wa Sudan. 

Mafunzo ya kazini kuhusu ufuatiliaji na udhibiti wa kesi za kipindupindu na magonjwa mengine ya kuambukiza pia yalifanywa huko Gedaref kwa wahudumu wa afya 185.

WHO inapeleka timu kusaidia

Hivi sasa, WHO imesema inatuma timu za kukabiliana na dharura ya mlipuko huo kwenye maeneo yaliyoathiriwa na inaunga mkono kwa dhati  na kusaidia wizara ya afya ya nchi hiyo katika kuhamisha sampuli za watu wanaoshukiwa kuwa na kipindupindu hadi kwenye maabara ya afya ya umma huko Port Sudan, kituo kilichowezeshwa na WHO kutoa huduma ya marejeleo ya kitaifa. 

Ufuatiliaji unaendelea katika maeneo yaliyoathirika na yenye hatari kubwa ili kutambua na kushughulikia mambo ya hatari. 

WHO pia imesema mipango imeanzishwa ili kuwezesha ombi kwa kikundi cha kimataifa cha uratibu wa utoaji wa chanjo ya kipindupindu ili kudhibiti Kipindupindu kwa njia ya  chanjo ya matone na kuweza kulinda idadi kuwa ya watu na kudhibiti mlipuko huo.

Kwa msaada kutoka kwa WHO na wadau wengine wa afya, wizara ya afya ya Sudan pia inaratibu juhudi za kuongeza upatikanaji wa maji safi na vifaa vya vyoo, pamoja na kuhakikisha jamii zilizoathiriwa na zilizo katika hatari zinafahamu hatari za maambukizi na mazoea sahihi ya usafi ili kupunguza hatari za uchafuzi na kuzuia kuenea zaidi kwa mlipuko huo.

Changamoto ya vita

Kutokana na vita iliyozuka mwezi Aprili 2023, Sudan inakabiliana na watu wengi waliokimbia makwao, milipuko ya magonjwa na utapiamlo, ambao umechangiwa na mvua kubwa na mafuriko. 

Mfumo wa afya umegubikwa na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na uhaba wa vifaa tiba na vifaa vingine, wahudumu wa afya na fedha za uendeshaji. Takriban 70% ya hospitali katika majimbo yaliyoathiriwa na mizozo hazifanyi kazi, huku hospitali na zahanati tendaji katika majimbo ambayo hayakuathiriwa na migogoro yamezidiwa na wimbi la wakimbizi wa ndani.