Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni dola bilioni 1 zinahitajika kusaidia mamilioni wanaokimbia mzozo wa Sudan - UNHCR

Mzozo nchini Sudan umewakosesha makazi maelfu ya watoto na familia zao.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Mzozo nchini Sudan umewakosesha makazi maelfu ya watoto na familia zao.

Sasa ni dola bilioni 1 zinahitajika kusaidia mamilioni wanaokimbia mzozo wa Sudan - UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), na mashirika 64 ya kibinadamu na kiraia leo Septemba 04 yametoa wito wa dola bilioni 1 kutoa msaada muhimu na ulinzi kwa zaidi ya watu milioni 1.8 wa Sudan wanaotarajiwa kuwasili katika nchi tano jirani ifikapo mwisho wa 2023, wakikimbia vita vinavyoendelea nchini mwao Sudan.

Hili ni ongezeko la mara mbili ya kile kilichokadiriwa hapo awali mwezi Mei kuhitajika kukabiliana na mzozo huo, huku uhamishaji na mahitaji yakiendelea kuongezeka. Zaidi ya wakimbizi milioni 1, waliorejea na raia wa nchi ya tatu tayari wameikimbia nchi. 

"Mgogoro huo umesababisha mahitaji ya dharura ya msaada wa kibinadamu, kwani wale wanaofika katika maeneo ya mipakani wanajikuta katika hali mbaya kutokana na huduma duni, miundombinu duni na ufikiaji mdogo," Mamadou Dian Balde, Mkurugenzi wa Ofisi ya UNHCR Kanda ya Mashariki na Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, na Mratibu wa Kikanda wa Wakimbizi kwa ajili ya Hali ya Sudan amesema akiongeza, "Washirika wanaoshiriki katika mwitikio huu wanafanya kila juhudi kusaidia wale wanaowasili na wenyeji wao, lakini bila rasilimali za kutosha za wafadhili, juhudi hizi zitapunguzwa sana." 

Mahitaji muhimu ni pamoja na maji, chakula, makazi, huduma za afya, msaada wa pesa taslimu, vitu muhimu vya usaidizi na huduma za ulinzi. 

Hasa, hali mbaya ya kiafya miongoni mwa wanaowasili inazidi kuwa ya wasiwasi na inahitaji uangalizi wa haraka. Viwango vya juu vya utapiamlo, milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na surua, na vifo vinavyohusiana na hilo vinatokea katika nchi kadhaa zinazopokea matibabu. 

"Inasikitisha sana kupokea ripoti za watoto wanaokufa kutokana na magonjwa ambayo yanazuilika kabisa, ikiwa wadau wangekuwa na rasilimali za kutosha, hatua haiwezi kucheleweshwa." amesema Balde. " 

Nchi zinazopokea watu wanaokimbia Sudan - Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini - zilikuwa zikipokea mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao hata kabla ya mgogoro huu. 

"Nchi katika eneo hili zinakabiliwa na changamoto kubwa zenyewe na bado zinaendelea kuonesha ukarimu wa ajabu, lakini hatuwezi kuchukua ukarimu wao kama kitu cha kawaida tu," anasema Balde.  

Anaongeza kusema, "Jumuiya ya kimataifa inahitaji kusimama katika mshikamano na serikali na jamii zinazowakaribisha na kushughulikia ufadhili mdogo unaoendelea wa shughuli za kibinadamu. Hii ni muhimu kusaidia watu binafsi na jamii zenye uhitaji, ikisubiri amani inayohitajika sana.” 

Mpango wa Kikanda wa kukabiliana na changamoto za wakimbizi (RRP) ulizinduliwa Mei 2023, ukarekebishwa Juni 2023, na tena mnamo Agosti 2023 kuakisi ongezeko kubwa na linaloendelea la wakimbizi kutoka Sudan na kusababisha janga la kibinadamu. Ingawa mahitaji yameongezeka kwa kasi, rasilimali za wafadhili hazijaendana na kasi. Hivi sasa, ni asilimia 19 tu ya mahitaji yaliyoongezeka ambayo yamepokelewa.