Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Sudan wafikia mil 4 mashirika ya UN yanafanya nini? 

Wakimbizi wanaokimbia Sudan wanajenga makazi ya muda katika mpaka na Sudan Kusini.
© UNHCR/Andrew McConnell
Wakimbizi wanaokimbia Sudan wanajenga makazi ya muda katika mpaka na Sudan Kusini.

Wakimbizi Sudan wafikia mil 4 mashirika ya UN yanafanya nini? 

Msaada wa Kibinadamu

Wakati idadi ya watu wanaokimbia machafuko nchini Sudan ikifikia milioni 4 mpaka sasa, mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yanafanya kila juhudi kuhakikisha wanawasaidia wale waliofanikiwa kukimbia machafuko na wale waliokwama nchini Sudan. 

Taarifa kutoka mashirika hayo zimeeleza pamoja na juhudi zinazofanywa lakini afya za wakimbizi zinazidi kuzorota, huduma muhimu za afya, maji na umeme hazipatikani, wafanyakazi wa afya wanauawa wakati wanatekeleza majukumu yao ya usaidizi wa kibinadamu na ufadhili wa ufadhili wa kuokoa maisha nao ukizidi kuchelewa.   

WHO 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO limetoa taarifa hii leo kutoka Geneva Uswisi likieleza pamoja na juhudi kubwa za kutoa usaidizi wa afya nchini humo lakini wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya matibabu pamoja na huduma nyingine muhimu kama maji na umeme katika maeneo yaliyoathirika na vita.   

WHO pia imelaani vikali mashambulizi yanayolenga vituo vya afya na wahudumu wa afya ambayo tangu tarehe 15 Aprili mpaka 31 Julai mwaka huu jumla ya vituo 53 vilikuwa vimeshambuliwa na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 38.   

“Mashambulizi dhidi ya huduma za afya ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki ya afya,” imesema taarifa hiyo ambayo imetaka wafanyakazi wa afya wahakikishiwe ulinzi na usalama.   

Mkimbizi ambaye alikimbia machafuko nchini Sudan kwa sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Gorom nchini Sudan Kusini.
© UNHCR/Charlotte Hallqvist
Mkimbizi ambaye alikimbia machafuko nchini Sudan kwa sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Gorom nchini Sudan Kusini.

UNHCR 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa afya za wakimbizi hao ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi.   

Sababu kubwa ya watu hawa kudhoofika ni kuwa safarini kwa wiki kadhaa huku wakiwa na chakula kidogo na hawana kabisa dawa.   

Utapiamlo ukiongezeka, mlipuko wa magonjwa na vifo navyo zinavidi kuongezeka ambapo kati ya tarehe 15 Mei na 17 Julai 2023 zaidi ya vifo 300, hasa miongoni mwa watoto walio chini ya miaka 5, viliripotiwa kutokana na surua na utapiamlo.   

Magonjwa kama kipindupindu na Malaria nayo yanazidi kuongezeka, ”Iwapo ufadhili wa programu za kuokoa maisha utaendelea kucheleweshwa, takwimu hii itaongezeka.” Imesema taarifa ya UNHCR.   

OCHA 

Pamoja na changamoto zote hizo misaada ya kibinadamu inaendelea kupelekwa nchini Sudan ikitokea nchini jirani ya Chad. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kibinadamu na kuratibu masuala ya dharura OCHA imesema katika jimbo la Darfur zaid ya watu 500,000 wamepatiwa msaada wa chakula tangu mwezi Mei 2023.   

Zaidi ya watu 15,000 walioko vijijini huko Darfur Magharibi nao wamfikishiwa misaada na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP

Kwa ujumla Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamepeleka wafanyakazi wa ziada na watu wa kujitolea katika kambi, vituo vya kuingia mpakani na vituo vya usafiri ili kusaidia uchunguzi wa utapiamlo na kutoa huduma nyinginezo.   

Pia wanaongeza kasi ya kutoa chanjo ya surua kwa watoto na kukarabati vituo vilivyopo huku wakijenga vipya ili kukabiliana na vifo vya watoto.   

Juhudi nyingine kadhaa ikiwemo kuwaondoa hataka watu katika kambi zilizosongamana zinafanyika ili kupunguza na kuzuia mlipuko wa magonwa ya kuambukiza.