Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu charipotiwa Kivu Kaskazini, DRC; UN na wadau wapeleka misaada

waziri wa afya akipatia mtoto dozi ya chanjo kwa uzinduzi katika kati ya wakimbizi wa ndani cha kanyaruchinya wilayani Nyiragongo-Goma
UN News/Byobe Malenga.
waziri wa afya akipatia mtoto dozi ya chanjo kwa uzinduzi katika kati ya wakimbizi wa ndani cha kanyaruchinya wilayani Nyiragongo-Goma

Kipindupindu charipotiwa Kivu Kaskazini, DRC; UN na wadau wapeleka misaada

Afya

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kumeripotiwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kuwa maeneo yaliyokumbwa zaidi na mlipuko huo ni Goma, Karisimbi, Masisi na Nyiragongo. 

“Mamlaka za afya zimesajili wagonjwa 1,800 waliothibitika kuambukizwa kipindupindu kati ya tarehe 13 na 19 mwezi huu wa Machi ikilinganishwa na wagonjwa 1,000 wiki iliyotangulia,” amesema Dujarric akinukuu wadau wa Umoja wa Mataifa wa operesheni za kibinadamu nchini DRC. 

Hadi sasa wagonjwa 6,200 wamethibitishwa 

Kwa ujumla amesema tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2023 hadi wiki iliyopita jumla ya wagonjwa 6,200 wamethibitishwa. 

Kwa mujibu wa Dujarric, maeneo hayo yenye mlipuko wa kipindupindu yanahifadhi zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 1 huku mazingira wanamoishi kwenye kambi yakiwa si safi kiafya. 

“Bila shaka tuna wasiwasi mkubwa juu ya changamoto wanayokabiliana nayo wakimbizi hao kupata huduma ya maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi,” amesema Dujarric akisema kuwa mazingira hayo ndio yanachochea kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu. 

Ukata unakwamisha operesheni za usaidizi 

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaendelea kutoa msaada kwenye vituo vya kutibu wagonjwa wa kipindupindu jimboni Kivu Kaskazini. 

“Ingawa hivyo vifaa vya msaada bado havitoshi na hali inaweza kuwa mbaya bila fedha za nyongeza ili kuharakisha hatua za usaidizi,” ametamatisha msemaji huyo wa UN. 

Kipindupindu DRC 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, kipindupindu ni ugonjwa unaoibuka mara kwa mara nchini DRC katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika ambako kila mwaka wagonjwa huripotiwa. 

Shirika hilo linatathmini mlipuko huo kuwa tishio kitaifa na kikanda na si kimataifa kwa kuzingatia hali tete ya amani kwenye maeneo ambako kipindupindu kinaripotiwa, mapigano na ukimbizi wa ndani, mlipuko wa magonjwa mengine na uhaba wa huduma za afya, maji safi na salama ya kunywa, huduma za kujisafi na mienendo ya watu kusafiri kutoka maeneo yenye ugonjwa kwenye nchi jirani kama vile Rwanda na Uganda.