Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC iko mbioni kuvunja rekodi ya ukiukwaji wa haki za watoto: UNICEF

© UNICEF/Jospin Benekire
Mama na watoto wake wakipita katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire

DRC iko mbioni kuvunja rekodi ya ukiukwaji wa haki za watoto: UNICEF

Haki za binadamu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, mwaka huu wa 2023 iko mbioni kuwa na viwango vya kuvunja rekodi vya ukiukaji mkubwa uliothibitishwa dhidi ya watoto kwa mwaka wa tatu mfululizo, kwa mujibu wa taarifa mpya iliyotolewa Alhamisi mjini Goma na shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

“Kuongezeka kwa ghasia, watu wengi kutawanywa, na ukaribu wa makundi yenye silaha kwa jamii kunasababisha ongezeko la kutisha la visa vya mauaji, ulemavu na utekaji nyara wa watoto nchini DRC. Mitindo huu ukiendelea, nchi iko mbioni kufikia viwango vipya vya juu vya ukiuwaji dhidi ya Watoto tangu utaratibu wa Umoja wa Mataifa wa ufuatiliaji na kuripoti uanze mwaka 2005, na kupita rekodi zilizowekwa mwaka 2022.” Limeongeza shirika hilo.

Takwimu za UNICEF zilizotolewa hivi karibuni zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 41 la idadi ya visa vya ukiukaji mkubwa uliothibitishwa dhidi ya watoto katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka mmoja uliopita. 

Pia kumekuwa na  visa 3,377 vya ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto 2,420 katika kipindi chote cha 2022, kulingana na Ripoti ya Katibu Mkuu ya Juni 2023 ya kuhusu watoto na migogoro ya silaha.

Matumizi ya watoto katika vita

Usajili na utumiaji wa watoto katika vikundi vyenye silaha umeongezeka kwa asilimia 45 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka limesema shirika hilo la Watoto la Umoja wa Mataifa. 

Mwaka 2022, watoto 1,545 wengine wakiwa na umri wa miaka 5 walithibitishwa kuwa waliandikishwa na kutumiwa na vikundi vyenye silaha. 

Mauaji na Watoto kulemazwa kuliongezeka kwa asilimia 32 katika kipindi kama hicho, ikilinganishwa na kesi 699 mwaka jana.

Ubakaji, vitendo vingine vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na utekaji nyara wa watoto pia viko kwenye viwango vya juu. 

Mwaka 2021 na 2022, DRC ilikuwa na viwango vya juu zaidi vya kesi zilizothibitishwa za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto uliofanywa na vikosi vya jeshi na vikundi vyenye silaha. 

Aidha, mwaka 2022, watoto 730 walithibitishwa kuwa walitekwa nyara, na kuifanya idadi kubwa zaidi ya utekaji nyara kuwahi kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Watu milioni 1.5 wamefurushwa makwao

Tangu ghasia kuzuka Oktoba 2022, watu milioni 1.5 wamelazimika kukimbia makazi yao ili kuokoa maisha yao mashariki mwa DRC, wakifurushwa kutoka kwenye makazi yao, maisha na jamii, na watoto mbali na shule zao. 

Kuna jumla ya watu milioni 6.1 waliokimbia makazi yao mashariki mwa DRC.

Katika kukabiliana na ongezeko la ukiukwaji wa haki na mahitaji ya dharura, UNICEF imetoa msaada kwa zaidi ya watoto 100,000 wa huduma za afya ya akili na kisaikolojia na imesaidia zaidi ya manusura 6,300 wa unyanyasaji wa kijinsia tangu mwanzoni mwa mwaka. 

Licha ya hayo, UNICEF imepokea asilimia 11 pekee ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na ulinzi wa watoto chini ya ombi la dharura la UNICEF mashariki mwa DRC, ikimaanisha kwamba mahitaji mengi hayafikiwi.