Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si hali Haiti, tuwasaidie polisi wa kitaifa - Türk

Watu waliohama makazi yao wakiwa katika uwanja wa ndondi katikati mwa jiji la Port-au-Prince baada ya kukimbia nyumba zao wakati wa mashambulizi ya magenge mnamo Agosti 2023.
© UNOCHA/Giles Clarke
Watu waliohama makazi yao wakiwa katika uwanja wa ndondi katikati mwa jiji la Port-au-Prince baada ya kukimbia nyumba zao wakati wa mashambulizi ya magenge mnamo Agosti 2023.

Hali si hali Haiti, tuwasaidie polisi wa kitaifa - Türk

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, hii leo ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa kusaidia ujumbe wa usalama kuwasaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) kupambana na vurugu zinazoendelea katika ngazi zote za jamii na kuzidisha hali mbaya ya usalama na ubinadamu pamoja na mgogoro wa haki.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo jijini Geneva Uswisi Kamishna Türk amesema “Kila siku maisha ya watu wa Haiti yanazidi kuwa magumu, lakini ni muhimu tusikate tamaa. Hali yao si ya kukatisha tamaa. Kwa msaada wa kimataifa na tukiamua, watu wa Haiti wanaweza kukabiliana na ukosefu huu mkubwa wa usalama, na kutafuta njia ya kutoka kwa machafuko haya.”

“Maisha ya watu yako hatarini,” Türk alisema. “Ni vyema kuzingatia muda - tunahitaji kuelewa maana ya dharura katika mgogoro huu.”

Baadhi ya wadau ikiwemo serikali ya Kenya imetangaza utayari wao wa kwenda kusaidia askari wa kitaifa wa Haiti kupambana na magenge ya wahalifu.

Ripoti kuhusu Haiti

Ripoti ya hivi karibuni ya Kamishna Mkuu huyo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Haiti imetilia mkazo kutumwa kwa ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama ili Kwenda kusaidia HNP katika kukabiliana na uhalifu uliopangwa, magenge yenye silaha na biashara ya kimataifa ya silaha, madawa ya kulevya na binadamu.

Mtaalamu Mteule wa Kamishna Mkuu kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Haiti, William O'Neill, alitembelea nchi hiyo mwezi Juni 2023 na katika taarifa yake ameeleza kushuhudia hali haliyo ilivyo na jambo la kwanza kabisa linalohitajia ni kuimarisha usalama.

Baada ya kurejea kutoka nchini Haiti O'Neill aliandika ripoti ambayo amesisitiza kwamba, "ujumbe wowote wa kimataifa wa usaidizi wa usalama lazima uzingatie sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, na kujumuisha taratibu za uangalizi wa ndaniza kuripoti utendaji na kuzuia na kukabiliana na unyonyaji na unyanyasaji wa kingono."

Wahaiti wapatao 200,000, hasa katika Port-au-Prince (pichani) wamelazimika kukimbilia maeneo ya muda  kwa sababu ya ukosefu wa usalama..
© UNOCHA/Giles Clarke
Wahaiti wapatao 200,000, hasa katika Port-au-Prince (pichani) wamelazimika kukimbilia maeneo ya muda kwa sababu ya ukosefu wa usalama..

Hali ikoje?

Ripoti inaeleza katika kipindicha kuanzia Januari 01 mpaka Agost 15, 2023 takriban watu 2,439 wameuawa, 902 kujeruhiwa na 951 kutekwa njara. 

Kuongezeka kwa vurugu tangu kuanza mwa 2023 tumeathiri jamii zote katika mji wa Port-au-prince ikiwemo maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yakitakwa kuwa ni salama. 

Magenge yameonesha unyama unaoongezeka, kwani wamekuwa wakiwakata watu viungo na kuchoma miili hadharani na kisha kusambaza picha hizo za kutisha kwenye mitandao ya kijamii.

Wanawake na wasichana wanakabiliwa na unyanyasaji unaotekelezwa na magenge hayo ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, kama vile wanawake kubwakwa na kikundi.

Magenge hayo yanayofanya vurugu yanaendelea kuajiri watoto na kuwatumia kama walinzi au wajumbe, na pia kuwahusisha katika utekaji nyara na wizi.

Ripoti inasema ukosefu wa usalama umezidisha mzozo wa kibinadamu ambao umefikia kiwango kipya zaidi ukilinganisha na miaka michache iliyopita. 

Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu imeongezeka karibu mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mashambulizi dhidi ya shule kutoka kwa washirika wa magenge yameongezeka mara tisa katika mwaka uliopita, na wafanyakazi wengi wa afya wameondoka nchini humo.

Wafungwa wanateseka

Hali ya wafungwa wa Haiti nayo inadhihirisha kuendelea kwa mmomonyoko wa utawala wa sheria. Ripoti hiyo inaeleza kuwa magereza ya Haiti ni ya kinyama

Mwishoni mwa Juni 2023, magereza ya Haiti ilikuwa ikiwashikilia wafungwa 11,810, idadi ambayo ni zaidi ya mara tatu ya uwezo wao. Takriban asilimia 85 ya walioshikiliwa walikuwa wafungwa kabla ya kesi yao kusikilizwa.

Wakati wa ziara yake kwenye Gereza la Kitaifa huko Port-au-Prince na Gereza Kuu la Cap-Haïtien, Mtaalamu Mteule William O'Neill aliona wafungwa wakiwa wamejazana kwenye jela ndogo, katika hali yenye joto, huku wakiwa na uwezo mdogo wa kupata maji na vyoo.

"Lazima wavumilie harufu ya kukosa hewa na, katika mji mkuu, vifusi vya takataka, ikiwa ni pamoja na kinyesi cha binadamu, vinaongeza uchafu. Wafungwa lazima wapokezane kulala kwa sababu hakuna nafasi ya kutosha ya kulala kwa wakati mmoja," alisema. Katika ripoti yake.

Ni kutokana an hali hizi ndio maana Kamishna Turk anahimiza hata baada ya usalama kurejea nchini Haiti kuna haja kubwa ya kusaidia katika maendeleo ya kiuchumi ya jamii pamoja na kuimaisha mifumo ya mahakama na haki. 

Kamishna Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka mamlaka husika nchini Haiti kusimamia kwa dhati matumizi ya fedha za umma ili kuzuia rushwa na kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na mahakama katika kuchunguza na kuwafungulia mashtaka washukiwa wa ufisadi.

Jamii za Port-au-Prince zimeweka vizuizi vya magari yaliyotelekezwa ili kupunguza hatari ya utekaji nyara na mashambulizi ya magenge.
© UNOCHA/Giles Clark
Jamii za Port-au-Prince zimeweka vizuizi vya magari yaliyotelekezwa ili kupunguza hatari ya utekaji nyara na mashambulizi ya magenge.

Ukweli kuhusu Haiti

Fahamu masuala kadhaa ya Haki za binadamu kutoka kwenye ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haiti iliyotolewa mwezi Septemba 2023

• Hali ya haki za binadamu inaangaziwa na mashambulizi ya kikatili, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela na utekaji nyara unaolenga raia.

• Vurugu za kutumia silaha na mashambulizi ya magenge ya wahalifu dhidi ya wananchi yanaongezeka.

• Magenge ya wahalifu yametumia wadunguaji wanaokaa juu ya paa kuwapiga watu risasi kiholela.

• Uporaji na uchomaji wa nyumba nyingi umesababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.

• Unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa vikundi, hutumiwa na magenge ya hawalifu kuwatia hofu hasa wanawake na wasichana.

• Kuibuka kwa vikundi vya sungusungu vya kizalendo kunaibua safu ya ziada ya utata katika hali ambayo tayari ina changamoto kubwa ya usalama.

• Taasisi za kitaifa hazina vifaa vya kuanzisha upya utawala wa sheria.

• Kuimarisha hali ya usalama nchini Haiti kutahitaji usaidizi mkubwa kwa polisi wa kitaifa.