Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njia pekee ya kutokomeza hatari ya nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia – Katibu Mkuu UN

Waandamanaji walitoa maoni yao kuhusu kutoeneza silaha katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. (Maktaba)
© ICAN/Seth Shelden
Waandamanaji walitoa maoni yao kuhusu kutoeneza silaha katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. (Maktaba)

Njia pekee ya kutokomeza hatari ya nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia – Katibu Mkuu UN

Amani na Usalama

Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kabisa Silaha za Nyuklia inatukumbusha kwamba wakati ujao wenye amani unategemea kukomeshwa kwa tishio la nyuklia, ndivyo António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyouanza ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii. 

Guterres anaona kwamba kutokuaminiana kijiografia na ushindani kumeongeza hatari ya nyuklia kwa viwango vya Vita Baridi. Wakati huo huo, maendeleo yaliyopatikana kwa bidii kwa miongo mingi ya kuzuia matumizi, kuenea na majaribio ya silaha za nyuklia yanabatilishwa.

“Katika Siku hii muhimu, tunathibitisha tena kujitolea kwetu kwa ulimwengu usio na silaha za nyuklia na maafa ya kibinadamu ambayo matumizi yake yanaweza kuzusha,” anasema kiongozi huyo wa Umoja wa Mataiafa na kuongeza kwamba hii ina maana kwamba, “Mataifa yenye silaha za nyuklia yaongoze kwa kutimiza wajibu wao wa kupokonya silaha, na kujitolea kamwe kutotumia silaha za nyuklia kwa hali yoyote.”

Inamaanisha kuimarisha kutokomeza silaha za nyuklia na kutoeneza silaha za nyuklia, ikiwa ni pamoja na kupitia Mikataba ya Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia na Marufuku ya Silaha za Nyuklia.

Inamaanisha nchi zote ambazo bado hazijaidhinisha Mkataba wa Marufuku ya Majaribio ya Nyuklia kufanya hivyo bila kuchelewa, na kwa yale Mataifa ambayo yanamiliki silaha za nyuklia kuhakikisha kusitishwa kwa majaribio yote ya nyuklia.

Inamaanisha kuzingatia mpangilio wa nyuklia unaobadilika na kushughulikia mistari mwembamba kati ya silaha za kimkakati na za kawaida na uhusiano na teknolojia mpya na zinazoibuka.

Zaidi ya yote, inamaanisha kutumia zana za wakati wote za mazungumzo, diplomasia na majadiliano ili kupunguza mivutano na kumaliza tishio la nyuklia. Muhtasari wa Sera uliozinduliwa hivi majuzi kuhusu Ajenda Mpya ya Amani unatoa wito kwa Nchi Wanachama kujitolea tena kwa haraka kwa sababu hii muhimu.

Bwana Guterres anahitimisha ujumbe wake akisema, "Njia pekee ya kutokomeza hatari ya nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia. Hebu tushirikiane kuviondoa vifaa hivi vya uharibifu kwenye vitabu vya historia, daima.”