Tuwasikilize na kupaza sauti kutetea haki za waathirika wa ugaidi: Guterres

20 Agosti 2021

Leo tarehe (21 Agosti) ni siku ya kumbukizi na kuwaenzi waathirika wa ugaidi duniani. 
Katika kuadhimisha siku hii, Umoja wa Mataifa unaungana na waathirika wote pamoja na jamii zilizo athirika na kuwapoteza wapendwa wao kutokana na vitendo vya kigaidi

Katika ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wanaunga mkono manusura wa ugaidi kwa kuwasikiliza wanapopaza sauti zao na kutetea haki zao pamoja na kutoa msaada na kuhakikisha wanapata haki zao wanazo stahili. 

“Mwaka huu tunapoadhimisha siku hii tukumbuke umuhimu wa kuwa na ukaribu na waathirika wa ugaidi hususan wakati huu wa janga la Corona au COVID-19 ambapo dunia bado inashuhudia vizuizi mbalimbali ikiwemo vya kutoka sehemu moja kwenda nyingine na watu kuonana au kukaa pamoja. Waathirika na manusura wanakosa fursa ya kukaa pamoja na kusaidiana.” Amesema Guterres.   
Pia ameeleza kitendo cha kuwa na ukaribu na waathirika na kushirikiana nao ni namna moja wapo ya kuwaponya  na kuwasaidia kupunguza machungu yaliyowazunguka na kunawafanya waone wanasikilizwa na hawapo pekeyao.

“ushirikiano baina ya manusura, waathirika, taasisi, asasi na jumiya mbalimbali ni muhimu zaidi kwa kuwa wadau hawa wanatoa msaada kwa waathirika wa sasa na wabaadae. Natarajia kuona namna tunavyoweza kushirikiana nao zaidi katika kongamano la waathirika wa ugaidi baadae mwaka huu”

Guterres amehitimisha ujumbe wake kwakusema kuwa Umoja wa Mataifa una dhamira ya dhati ya kuona ulimwengu usio na vitendo vya ugaidi. 

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa jamii inatakiwa kuwakumbuka waathirika wa ugaidi si leo pekee bali siku zote na kuhakikisha wanashikamana nao kutetea haki zao na kusikiliza simanzi wanazozipata kila wakumbukapo madhila ya kigaidi yaliyowakumba na kuhakikisha wanawapa matumaini na kuwasaidia kuponya hofu walizonazo.
 

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter