Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atua Haiti kuhimiza mshikamano wa kimataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake huko Port-au-Prince nchini Haiti.
Oldy Joël Auguste/BINUH
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake huko Port-au-Prince nchini Haiti.

Katibu Mkuu wa UN atua Haiti kuhimiza mshikamano wa kimataifa

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasili katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince hii leo kwa ajili ya kuonesha mshikamano na watu wa Haiti, ambao wanapitia mfululizo mbaya wa majanga ya usalama, kisiasa na kibinadamu. 

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wake jijini New York Marekani leo, imesema katika ziara yake hiyo, “Katibu Mkuu atakutana na Waziri Mkuu Ariel Henry na atasikiliza kutoka kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa, Baraza Kuu la Mpito, wanachama wa mashirika ya kiraia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.” 

Taarifa hiyo imeeleza zaidi kuwa akiwa Port-au-Prince, Katibu Mkuu atasisitiza uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa Haiti, wito wake mkubwa kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kusaidia Haiti na mahitaji yake ya kibinadamu, pamoja na wito wake wa kutumwa mara moja kwa kikosi cha kimataifa kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti.  

Tweet URL

Katika ukurasa wake wa Twitter Guterres anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono uundaji wa kile alichokiita "kikosi chenye nguvu cha kimataifa" kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti.

Pia akiwa Haiti atasisitiza haja ya kuwa na njia ya kisiasa inayoongozwa na Haiti, inayojumuisha watu wote kuelekea uchaguzi na kurejea kwa utaratibu wa kikatiba nchini Haiti. 

Usaidizi wa kikanda na jukumu la CARICOM 

Katika ziara hiyo rasmi, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amekutana na Waziri Mkuu Ariel Henry, wanachama wa mashirika ya kiraia na Baraza Kuu la Mpito, pamoja na vyama vya kisiasa na maafisa wa Umoja wa Mataifa. Kwa Guterres, ni muhimu kuunda muungano wa kisiasa ili kumaliza migogoro. 

Guterres amepongeza mazungumzo ya Haiti yanayoandaliwa na Jumuiya ya soko la pamoja la nchi za ukanda wa Karibea, CARICOM kwa lengo la kufikia makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. 

Kulingana na Guterres, ni muhimu kujumuisha wanawake na vijana katika mchakato huu. Amesisitiza kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, BINUH, inaendelea kuunga mkono juhudi hizi. 

Alipokutana na wanawake na vijana wa Haiti, Guterres amesema amehisi uchovu wa watu kutokana na hali mbaya ya Haiti. “Leo, mmoja kati ya Wahaiti wawili anaishi katika umaskini uliokithiri akiteseka kwa njaa na ukosefu wa maji safi.” 

Mpango wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa umepokea tu 23% ya kiasi kilichoombwa hadi sasa. 

António Guterres amehitimisha kwa kusema kwamba hakuna suluhu kwa Haiti inayoweza kupatikana bila watu wa Haiti, ambao wanastahili mustakabali salama na wa haki.