Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dunia na ahadi mpya ya kutokomeza TB

Mgonjwa wa TB akiwa anaendelea na matibabu nyumbani  nchini Colombia.
© PAHO/Joshua Cogan
Mgonjwa wa TB akiwa anaendelea na matibabu nyumbani nchini Colombia.

Viongozi wa dunia na ahadi mpya ya kutokomeza TB

Afya

Vifijo na nderemo vilisikika kwenye moja ya kumbi za mikutano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo baada ya wawakilishi wa serikali, wataalamu wa afya na wawakilish iwa mashirika ya kiraia kupitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kutokomeza Kifua Kikuu au TB ifikapo mwaka 2030 ambapo pamoja na mambo mengine linalenga kufikia asilimia 90 ya watu na huduma za kinga na tiba dhidi ya TB.

Waliopitisha azimio hilo ni viongozi wa dunia waliokutana jijini New York, Marekani kwenye mkutano wa ngazi ya  juu y kuhusu TB, mkutano ulioandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO.

Aliyepona TB asimulia unyanyapaa aliokumbana nao

Mwandishi wa vitabu nchini Mongolia, Handaa Rea, ambaye amepona TB alishiriki mkutano huo na kusihi viongozi wa dunia kutibu TB kama sio tu ugonjwa bali pia suala la kijamii.

Ameandika kuhusu  uzoefu wake wa unyanyapaa utokanao na kuugua TB, ikiwemo kubaguliwa ambako amesema kumeenea hasa katika nchi zinazoendelea na hivyo kusababisha mamia ya maelfu ya watu kuchelewa kusaka matibabu.

Madhara ya unyanyapaa ni makubwa zaidi kwa wanawake na wasichana ambao wanatakiwa kuwa na viwango vya juu vya afya, ustawi na urembo, amesema Bi. Rea.

“Pale jamii inaposema vitu kama vile, ‘ni mwembamba  mno, kwa sababu ana TB, hana thamani ya kuolewa kwa sababu ana TB, au anaendelea kuugua TB kwa sababu hawajibiki,’ sisi kama jamii tunawaonea wagonjwa wa TB na kuwasogeza karibu na kifo, kifo ambacho kinaweza kuepukika, na hii lazima ikome,” amesema.

Fahamu malengo mapya ya miaka 5

Malengo hayo, kwa mujibu wa azimio hilo ni ya kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa ambapo nchi zitatumia vitendanishi vipya vya WHO vya kupima haraka ugonjwa wa TB; kuwapatia wagonjwa wa TB marupurupu ya kijami; kuidhinisha angalau chanjo mpya dhidi ya TB na kufunga pengo la ufadhili wa fedha kwa ugonjwa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya TB, halikadhalika utafiti ifikapo mwaka 2027.

“Kwa zama na zama, mababu zetu wametatizika na hata kufa kutokana na TB bila kufahamu ilikuwa ni nini, ilisababishwa na nini na  hata jinsi ya kuutokomeza,” amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus kwenye mkutano huo.

Amesema leo hii “tuna ufahamu na mbinu ambazo watangulizi wetu waliweza kuota tu. Azimio hili la kisiasa lililopitishwa na nchi hii leo, na malengo ambayo limeweka, ni ahadi ya kutumia mbinu hizo, kuendeleza mbinu mpya na hatimaye kufunga kabisa ukurasa wa TB.”

Chanjo ya sasa dhidi ya TB haina kinga fanisi kwa barubaru na watu wazima

Kwa sasa BCG ni chanjo pekee iliyoidhinishwa dhidi ya TB. WHO inasema ingawa ina ufanisi wa kiwango cha kati kwenye kinga kwa watoto wachanga na watoto, bado haina kinga thabiti kwa barubaru na watu wazima ambao ndio wanachangia asilimia takribani 90 ya maambukizi ya ugonjwa huo duniani.

Malengo ya 2018 hayakutimia ipasavyo: COVID19 na mizozo ni sababu

Malengo ya azimio la kisiasa la mwaka 2018 yametimizwa kwa kiasi gani? Hilo ni moja ya maswali ambayo washiriki wa mkutano huo walitolea majibu ambapo WHO inasema kuwa juhudi za kimataifa za kutokomeza TB zimeokoa maisha ya zaidi ya watu milioni 75 tangu mwaka 2000, idadi ambayo hata hivyo haikufikia lengo lililokuwa limewekwa. 

coronavirus">COVID-19, majanga na vita vilivuruga huduma za TB ambapo ni wagonjwa milioni 34 pekee wa TB kati ya walengwa milioni 40 ndio walifikiwa na matibabu kati ya 2018 na 2022.

Huduma za kinga dhidi ya TB zilikumbwa na kiza zaidi kwani ni watu milioni 15.5 tu kati ya walengwa milioni 30 ndio walifikiwa na huduma za kinga.

Ufadhili wa huduma za TB kwa nchi za kipato cha chini na cha kati uliporomoka kutoka dola bilioni 6.4 mwaka 2018 hadi dola bilioni 5.8 mwaka 2022, ikiwa ni pengo la asilimia 50 la ufadhili wa TB.

Utafiti nao kwa mwaka kwa ajili ya kutokomeza TB ulikuwa kati ya dola bilioni 0.9 hadi dola bilioni 1.0 kati ya 2018 na 2022, kiwango ambacho ni nusu ya lengo lililowekwa mwaka 2018.

WHO inasema hali hiyo inaongeza mzigo mzito zaidi kwa wagonjwa hasa walio  hatarini zaidi.

Leo hii TB inasalia kuwa moja ya magonjwa ya kuambukiza yanayoongoza kwa vifo duniani ambapo kila mwaka zaidi ya watu milioni 10 wanaugua na kati yao hao zaidi ya milioni 1 wanakufa kwa ugonjwa huo wenye kinga na tiba.