Ethiopia yazindua mwongozo mpya wa kuwafikia wagonjwa wa Kifua kikuu.

27 Disemba 2018

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO nchini Ethipoia, linasema linaazimia kufanikisha lengo lake la kuona ugonjwa wa kifua kikuu, TB, hausambai ifikapo mwaka wa 2035 na pia kuutokomeza kabisa ifikapo mwaka wa 2050 nchini humo.

Afisa wa kitaifa anayehusika na kifua kikuu katika ofisi ya WHO nchini Ethiopia, Dkt Ismail Hassen, ametoa kauli hiyo mjini Addis Ababa katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya mratibu wa magonjwa ya kuambukiza nchini Ethiopia, Dkt Esther Aceng-Dotum, wakati wa uzinduzi wa mwongozo mpya wa kuwafikia  wagonjwa wa kifua kikuu nchini humo ambao hawakufikiwa katika awamu iliyopita.

Amesema kuwa WHO ikishirikiana na wadau wengine kama vile ofisi za afya za kikanda pamoja na wizara husika itaendelea kuunga mkono mpango wa kitaifa kuhusu kifua kikuu ili kufanikisha lengo la kuutokomeza ugonjwa huo.

Ethiopia ni moja ya nchi 30 duniani ambazo zina mzigo mkubwa wa kifua kikuu kikiwemo kifua kikuu ambacho ni sugu dhidi ya dawa. Ripoti ya dunia kuhusu kifua kikuu ya mwaka 2018, iliorodhesha visa 117,705 vya kifua kikuu nchini Ethiopia ambapo matibabu ya ugonjwa huo usio sugu kwa dawa ni asilimia 68, huku  asilimia 25 tu ya wagonjwa wenye kifua kikuu sugu ndiyo walipatakiana na kutibiwa.

WHO inatoa msaada wa kiufundi kwa wizara za afya za kikanda kwa kusaidia upatikanaji wa dawa inayofaa pamoja na mbinu za kuboresha matibabu.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la WHO, kifua kikuu kinashika nafasi ya tisa kati ya magonjwa yanayosababisha vifo vya watu wengi duniani. Mwaka wa 2016 watu milioni 2.5 waliugua kifua kikuu barani Afrika, hiyo ikiwa ni sehemu ya robo ya wagonjwa wote wa kifua kikuu duniani kote. Mwaka 2016 takriban watu 417,00 katika kanda ya Afrika na watu milioni 1.7 duniani kote walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo takwimu za WHO zinaonesha  katika yam waka 2000 ma 2015 takriban watu milioni 53 duniani kote waliokolewa kutokana na kifua kikuu, milioni 10 kati yao wakiwa barani Afrika. 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud