Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kama COVID-19 ilivyotiliwa mkazo ifanyike hivyo kwa Kifua Kikuu

Waziri wa Afya wa Kenya Susan Nakhumicha Wafula.
UN News
Waziri wa Afya wa Kenya Susan Nakhumicha Wafula.

Kama COVID-19 ilivyotiliwa mkazo ifanyike hivyo kwa Kifua Kikuu

Afya

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mapambano dhidi ya kifua kikuu au TB ukifanyika leo hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, Waziri wa Afya wa Kenya Susan Nakhumicha Wafula amesema kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030 inawezekana endapo Dunia itashikama na kuweka msokumo mkubwa kwa ugonjwa huo kama ilivyofanya wakati wa mlipuko wa janga la COVID-19.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Waziri Wafula amesema “Najiuliza, mbona sisi watu wote, kwanza wafadhili na wale wazalishaji wa hizo dawa na vifaa, mbona tusifikirie lile jambo moja ambalo tunastahili kufanya ili kumaliza ugonjwa wa TB?” 

Akifafanua zaidi Waziri huyo amesema jambo la muhimu ni kupata kinga ili watu wasipata ugonjwa wa TB kwakuwa kwa kiasi kikubwa wanaoambukizwa ni watu walio katika maeneo duni. 

“Kulikuwa na COVID-19, muda mfupi tu kumekuwa na chanjo na sasa watu tunatembea kwa uhuru kabisa na watu wanatangamana, pale mwanzo COVID-19 ilikuwa imefanya watu hawatembeleani. Ninauhakika kwamba tukiweka fedha kwenye sayansi, kufanya utafiti na maendeleo tutapata chanjo ya hii TB ama pia tupate tiba ya mara moja.”

Waziri huyo wa Afya kutoka nchini Kenya amesema pamoja na taifa hilo kutibu ugonjwa wa TB bure kwa wananchi wake lakini changamoto wanayokutana nayo ni uhaba wa vifaa tiba katika baadhi ya hospitali na kutoa wito kwa wafanyabiashara kupunguza bei za vifaa tiba hivyo ili waweze kusambaza katika hospital zote nchini Kenya.  

Kuhusu namna watakavyotekeleza Azimio la kisiasa kuhusu Afya kwa wote nchini Kenya ambayo wanaiita “Afya Mashinani” Waziri Wafula amesema Kenya imejipanga kutekeleza katika vipengele vifuu vinne ambavyo ni: kuhakikisha kuna dawa na vifaa tiba, kuhakikisha kuna watoa huduma katika vituo vya afya, matumizi ya teknolojia kufikisha afya mashinani na ufadhili wa afya kupitia bima ya afya ya taifa.