Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wito wa dhamira na utashi wa viongozi watawala ufunguzi wa Mjadala Mkuu UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa ufunguzi wa mjadala mkuu.
UN News/Anton Upenskiy
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa ufunguzi wa mjadala mkuu.

Wito wa dhamira na utashi wa viongozi watawala ufunguzi wa Mjadala Mkuu UN

Masuala ya UM

Mwanzo wa mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au UNGA78 umeanza na wito wa mageuzi ya ushirikiano wa kimataifa ili kuzuia "mgawanyiko mkubwa" kati ya nchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis wametumia hotuba zao za ufunguzi leo Jumanne jijini New York kusisitiza kwamba uwezo na njia za kutatua changamoto zipo, lakini hatua hazipo.

Viongozi kadhaa wa dunia leo wameendelea kumiminika mjini New York, Marekani kwa ajili ya kuanza kwa mijadala ya ngazi ya juu kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa.

Katika ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa, "ulimwengu unahitaji watu wa serikali na sio michezo au migogoro". 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kwenye ufunguzi wa mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kwenye ufunguzi wa mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kiongozi huyo amerejelea kwamba dhamira iko katika vinasaba vya Umoja wa Mataifa na ni neno lililopo sana katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katibu mkuu amesema kwamba "tuna zana na rasilimali zote za kutatua changamoto za pamoja, tunachohitaji ni uamuzi."

Rais wa UNGA78

Naye Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu, Dennis Francis, amesema kwamba, mwaka huu, jambo la lazima ni kuunganisha mataifa “katika imani ya kusudi moja na mshikamano wa hatua za pamoja".

Akizungumzia athari za kimataifa za vita vya Ukraine, Balozi Francis amesema kwamba ni muhimu kukumbuka kuwa, "amani ni uwekezaji katika ustawi wetu wa pamoja".

Amesisitiza kuwa vita, mabadiliko ya tabianchi, madeni, majanga ya chakula na nishati, umaskini na njaa vinaathiri ustawi wa mabilioni ya watu.

Baadaye zimefuata hotuba za wakuu wa nchi na serikali ambapo Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva ameanza akifuatiwa na Rais mwenyeji, Joe Biden wa Marekani.