Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa uaminifu na mshikamano unachelewesha Ajenda 2030 – Rais Nyusi wa Msumbiji

Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 cha Baraza Kuu.

Ukosefu wa uaminifu na mshikamano unachelewesha Ajenda 2030 – Rais Nyusi wa Msumbiji

Masuala ya UM

Amani na usalama, kupambana na ugaidi, mabadiliko ya tabianchi, kubadilisha nishati, uchumi wa bluu na uhifadhi wa mazingira vimekuwa vipaumbele vya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alipohutubia katika siku ya kwanza ya mjadala mkuu wa UNGA78 jijini New York, Marekani.

Filipe Nyusi ameanza hotuba yake kwa kusema kwamba viongozi wa dunia wamejitolea kupunguza umaskini katika maeneo 17 muhimu, hata hivyo, "ulimwengu unaendelea kukabiliwa na migogoro kadhaa iliyofungamana ambayo inahatarisha mafanikio ya Ajenda ya 2030."

"Kwa kweli, janga la Covid-19, majanga ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya silaha, pamoja na ugaidi na itikadi kali, inamaanisha kuwa mamilioni ya watu wanaendelea kuishi katika umaskini, bila chakula cha kutosha, bila kupata huduma za afya na elimu. ”

Kiongozi huyo wa Msumbiji amesisitiza "kutokuwepo kwa uaminifu na mshikamano kati ya walenacho na wale ambao wana kidogo au karibu hawana chochote" kama sababu ya kushindwa kwa Ajenda ya 2030.

Kuhusu suala la ugaidi, Nyusi amesema wakati huo huo Msumbiji inataka kufunga ukurasa wa mchakato wa amani na maridhiano ya kitaifa, "inakabiliwa na hali mbaya ya ugaidi, hasa jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mwa Nchi."

Ametaja ushirikiano wa kimataifa na kikanda kuwa ni sababu zinazochangia mafanikio ya juhudi za kukabiliana na ugaidi lakini akazua wasiwasi kuhusu uendelevu wa operesheni.

Rais Nyusi ameainisha mabadiliko ya tabianchi kama "janga kuu la wanadamu katika karne hii."

Amesisitiza kuwa nchi, kwa sababu ya eneo lake la kijiografia, "kwa mzunguko hukabiliwa na athari mbaya za majanga ya asili."

Kwa mujibu wa Nyusi, vimbunga vikubwa vya mwisho hivi karibuni, Idai, Keneth na Freddy, vilisababisha mamia ya vifo na hasara na uharibifu wa mabilioni ya dola. "Kufikia sasa, hatujaweza kurejesha hata theluthi moja ya uharibifu uliorekodiwa," amesema.

Rais wa Msumbiji amesisitiza kuwa kubadilika kwa nishati kunahitaji uwekezaji mkubwa katika miradi ya kuzalisha nishati kutoka kwa vyanzo safi.

Kwa mantiki hii, amesisitiza ombi la nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda kuonesha mshikamano, na kuongeza ufadhili wa tabianchi.

Nyusi pia amesema kuwa Msumbiji inaamini katika maendeleo ya uchumi wa bluu ili kuongeza rasilimali za ukanda wa kipekee wa kiuchumi kwenye ukanda wa pwani wa kilomita 2,700.