Skip to main content

Turejee kwenye mazao ya asili yaliyopuuzwa

Kikundi cha Amaati kinawawezsha wanawake wa kijijini nchini Ghana kupitia kilimo cha mazao ya asili kama fonjo
© Amaati Group
Kikundi cha Amaati kinawawezsha wanawake wa kijijini nchini Ghana kupitia kilimo cha mazao ya asili kama fonjo

Turejee kwenye mazao ya asili yaliyopuuzwa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tarehe 17 na 18 Septemba yani leo na kesho hapa katika makao Makuu viongozi wanakutana kuangalia vipi wametekeleza malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs ambayo yanatarajiwa kufikia kilele mwaka 2030. 

Wadau wa Maendeleo wamejaa hapa katika makao Makuu hakika na rangi za malengo 17 zikiwa zimetaradadi kila kona kuanzia nje mpaka ndani ya Baraza Kuu, mwaka huu wakija na maudhui yasemayo, Kujenga upya kuaminiana na kuchochea mshikamano wa dunia.

Mikutano ya SDGs imekuwa na ubunifu tofauti mwaka baada ya mwaka, na mwaka huu katika eneo la wazi baada tu ya kuingia makao makuu kuna milango midogo 17 inayoonesha malengo 17 na kila mlango una mchechemuzi na umeandikwa namna anavyopambana kutekeleza lengo.

Mlango namba mbili ni kutokomeza njaa, na ukifungua mlango unakutana na Pierre Thiam raia wa Senegali na mpishi mwenye makazi yake hapa jijini New York Marekani, yeye anaamini kuwa dunia inaweza kutokomeza njaa iwapo itageukia katika mazao ambayo hayatumiwi sana na yamekuwa yakipuuzwa.

Thiam alihojiwa na mwenzangu Florence Westergard wa Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa na anasema,“Kwa hiyo kupambana na njaa kutanza kwa kubadili mifumo yetu ya chakula na kurejea katika aina ya kilimo kinachosaidia wakulima wadogo na mazao yao ambayo hayatumiki, na kutafuta njia za kuongeza thamani katika mazao hayo na kuyafanya yaweze kupatikana masokoni.”

Thiam yeye ananena na anatenda kwani anahamasisha zao la Forno ambalo linapatikana maeneo mengi ya ukanda wa Sahel. Ukanda ambao nchi nyingi zinatakabiliwa na uhaba wa chakula.

Kwakweli Flora mara baada ya kumsikia mchechemuzi huyu nami nikakumbuka kule kwetu Kilimanjaro Tanzania tumehamasika kula ndizi lakini kuna mazao kama viazi vikuu ambavyo ndio hayo yanayoelezwa kuwa yamepuuzwa na tunapaswa kurejea kwayo.