Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA78: ‘Ulimwengu unahitaji vitendo’ – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Hali mbaya ya tabianchi Sudan Kusini inaharibu maisha ya baadhi ya watu walio hatarini zaidi duniani.
© UNICEF/Sebastian Rich
Hali mbaya ya tabianchi Sudan Kusini inaharibu maisha ya baadhi ya watu walio hatarini zaidi duniani.

UNGA78: ‘Ulimwengu unahitaji vitendo’ – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Jumatano ametuma ujumbe wa wazi kwa viongozi wa dunia wanaowasili New York wiki ijayo kwamba: "Huu sio wakati wa kujipanga bali ni wakati wa kuchukua hatua." 

"Huu sio wakati wa kutojali au kutokuwa na uamuzi", António Guterres amewaeleza waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. "Huu ni wakati wa kukusanyika kwa ajili ya suluhisho la kweli na la vitendo." 

'Maelewano kwa ajili ya kesho bora' 

"Ni wakati wa maelewano kwa ajili yakesho bora. Siasa ni maelewano. Diplomasia ni maelewano. Uongozi bora ni maelewano.” 

Kiongozi huyo ameanza hotuba yake akitafakari kuhusu maelfu ya vifo nchini Morocco na Libya katika siku za hivi karibuni. 

"Umoja wa Mataifa unahamasisha kuunga mkono juhudi za misaada. Tutafanya kazi kwa njia yoyote na kila tuwezavyo na washirika kusaidia kupata msaada wa dharura kwa wale ambao wana uhitaji mkubwa”, amesema Katibu Mkuu. 

Akiwa ndio kwanza ametoka katika mikutano mikuu ya kimataifa huko Nairobi, Jakarta na New Delhi - pamoja na ziara ya Havana siku ya Alhamisi kukutana na viongozi wa kundi la G77 pamoja na China - amesema UNGA78 imeitisha mikutano ya ngazi ya juu huku kukiwa na changamoto kubwa. 

Ametoa mfano wa dharura ya tabianchi inayoongezeka, migogoro mipya, gharama ya maisha, na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa. 

Tutoeni kwenye changamoto hii 

“Watu wanawatazamia viongozi wao kwa ajili ya njia ya kutoka katika hali hii mbaya. Hata hivyo kutokana na haya yote na zaidi, migawanyiko ya kijiografia inadhoofisha uwezo wetu wa kutatua”, amesema Bwana Guterres. 

"Ulimwengu wenye mataifa mengi yenye nguvu sawa unaibuka. Hali hii inaweza kuwa sababu ya usawa, lakini inaweza pia kusababisha mvutano kuongezeka, kugawanyika na mbaya zaidi." 

Ili kuimarisha utaratibu huu mpya na tata wa dunia, kunahitajika kuwa na taasisi imara na zilizofanyiwa marekebisho kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. 

"Ninajua mageuzi kimsingi yanahusu mamlaka - na kuna maslahi na ajenda nyingi zinazoshindana katika ulimwengu wetu unaozidi kuwa na nchi nyingi", ameendelea. 

Wiki ijayo inaanza na mkutano wa siku mbili kuhusu jinsi bora ya "kuokoa" Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyokubaliwa huko Paris miaka minane iliyopita, kuelekea tarehe ya mwisho ya 2030. 

Akimalizia mazungumzo yake mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amerejelea ombi lake kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoelekea Manhattan: 

"Ikiwa tunataka mustakabali wa amani na ustawi unaozingatia usawa na mshikamano, viongozi wana jukumu maalum la kufikia maelewano katika kubuni mustakabali wetu wa pamoja kwa manufaa yetu sote." 

"Wiki ijayo jijini New York ndio mahali pa kuanzia." Amesema Guterres.